WHO: Mpox sio tena dharura ya afya ya kimataifa
5 Septemba 2025Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kwamba uamuzi huo umezingatia ushauri wa Kamati ya Dharura ya WHO, ambayo hukutana kila baada ya miezi mitatu kutathmini hali ya mripuko.
Amesisitiza kuwa ingawa hali ya dharura imeondolewa, hali hiyo haimaanishi kuwa tishio la Mpox limekwisha kabisa, wala juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zimesitishwa.
WHO imesema kuwa hatua hiyo ni ishara ya mafanikio ya juhudi za kimataifa za kudhibiti ugonjwa huo, lakini pia ni wito wa kuendelea kuwa waangalifu na kuimarisha mifumo ya afya ili kuzuia miripuko ya baadaye.
Ugonjwa wa Mpox ulitangazwa kuwa dharura ya afya ya kimataifa kwa mara ya kwanza mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita, kufuatia mripuko mpya ulioripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kusambaa kwa kasi katika nchi jirani za Burundi, Sierra Leone na Uganda.