WEIMAR: Miaka 60 tangu kukombolewa kwa kambi ya Buchenwald
10 Aprili 2005Wanasiasa mashuhuri wa Ujerumani hii leo walikusanyika na zaidi ya wageni 1,000 katika mji wa mashariki Weimar kuadhimisha mwaka wa 60 tangu kukombolewa kwa kambi ya Buchenwald.Miongoni mwa wageni waliokuwepo ni kiasi ya watu 500 waliookolewa kutoka kambi hiyo.Pia walikuwepo wanajeshi 50 wa zamani wa Kimarekani waliokuwa sehemu ya vikosi vilivyosaidia kuikomboa kambi ya Buchenwald.Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani alikuwa kiongozi wa kwanza kuwahotubia wageni kutoka nchi 26.Katika hotuba yake Schroeder amesema viongozi wanaoiwakilisha Ujerumani iliyo tofauti na ya udemokrasia,watahakikisha kuwa udhalimu,utumiaji wa nguvu,ubaguzi wa kikabila na wa Wayahudi ni mambo ambayo kamwe hayatopata nafasi ya kujitokeza.Buchenwald ilikuwa kambi ya kwanza ya Manazi kukombolewa na majeshi ya madola shirika tarehe 11 April,mwaka 1945.Kiasi ya wafungwa 21,000 waliokolewa kutoka kambi hiyo,lakini zaidi ya 56,000 walikufa.