Waziri Wang Yi wa China kufanya ziara Urusi wiki ijayo
28 Machi 2025Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Guo Jiakun, ameelezea dhumuni ya ziara hiyo:
"Katika ziara hiyo, Waziri Wang Yi atakutana na viongozi wa Urusi na kufanya mazungumzo na mwenzake Sergei Lavrov. China inazingatia ziara hii kama fursa ya kufanya kazi na Urusi ili kuwezesha utekelezaji wa makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizi mbili na kuwa na mawasiliano ya kina kuhusu mustakabali wa mahusiano kati ya China na Urusi, pamoja na masuala ya kimataifa na kikanda ambayo yanagusa pande zote mbili."
Siku ya Alhamisi, akiwa mjini Beijing, mwanadiplomasia mkuu wa UfaransaJean-Nöel Barrot alimweleza Wang Yi kwamba China ina jukumu la kuishawishi Urusi kuja kwenye meza ya mazungumzo ikiwa na mapendekezo yenye tija na yanayodhihirisha nia njema.
Putin: Ukraine iwekwe chini ya utawala wa muda
Rais wa Urusi Vladimir Putin amependekeza kuwa Ukraine inapaswa kuwa chini ya utawala wa muda ili kuruhusu uchaguzi mpya na kuwezesha makubaliano muhimu ya kufikia suluhu katika vita hivyo. Kauli ya Putin aliyoitoa alipotembelea bandari ya kaskazini ya Murmansk, inajiri huku Marekani ikiendelea na juhudi za usuluhishi kwa kufanya mazungumzo tofauti na pande hizo mbili.
Rais huyo wa Urusi amekuwa akishutumiwa na Ukraine pamoja na viongozi wa Ulaya wanaosema kuwa anajaribu tu kurefusha mazungumzo ya kusitisha mapigano bila ya kuwa na nia yoyote ya dhati ya kusitisha kabisa vita hivyo ambavyo vimesababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na maelfu ya vifo, mamilioni ya wakimbizi huku miji kadhaa ikigeuzwa kuwa magofu.
Soma pia: Ukraine na Urusi zaendelea kutupiana lawama
Pendekezo la Putin la uwepo wa utawala wa muda nchini Ukraine linaakisi malalamiko yake ya muda mrefu ambapo alikuwa akisema kuwa viongozi wa sasa si washirika halali wa mazungumzo hasa Rais Volodymyr Zelensky ambaye amesalia madarakani hata baada ya muhula wake kumalizika mwezi Mei mwaka 2024.
Hayo yakiarifiwa, Urusi iliishambulia Ukraine na kuharibu maghala ya kampuni ya uzalishaji wa gesi katika eneo la Poltava, huku jeshi la anga la Ukraine likisema limedungua droni 89 kati ya 163 zilizorushwa na Moscow. Wakati huohuo, Urusi imeilaumu Ukraine kuwa inaendelea kushambulia miundombinu yake ya nishati.
(Vyanzo: AP, AFP, DPA)