Waziri wa ulinzi wa Ujerumani ziarani nchini Afghanista
27 Septemba 2004Uwezekano kama huo anaotafuta waziri wa ulinzi Peter Struck umepangwa kujadiliwa alkhamisi ya wiki hii kwenye kikao cha bunge mjini Berlin, baada ya baraza la mawaziri kuidhinisha wiki iliyopita haja ya kurefushwa muda wa askarijeshi wa kutunza amani wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr nchini Afghanistan hadi mwezi oktoba mwaka ujao wa 2005. Jeshi la kutunza amani la kimataifa ISAF, linatakiwa lisivuke idadi ya askarijeshi 2 250. Mpango unaohusika unasema 45o kati yao watarundikwa katika eneo la Kundus. Kuna haja ya kurefushwa muda wa wanajeshi hao, kwani dhamana yao ya sasa inahitimika tarehe 13 mwezi ujao wa oktoba.
Wakati wa ziara yake katika maeneo ya kaskazini mwa Afghanistan ya Kundus na Feisabad, waziri Struck pamoja na wanajeshi wake walikubaliana kwa kauli moja kwamba, mchango unaotolewa sasa na wanajeshi hao, unahitajiwa sana na Afghanistan katika ujenzi upya na katika kuimarisha demokrasia, isitoshe, unatukuza haiba ya Ujerumani duniani. Waziri wa ulinzi Struck kwa ziara yake alidhamiria hasa kuwatia moyo ana kwa ana wanajeshi wake. Sababu mojawapo ni kwamba, siku chache baada askarijeshi 66 wa Ujerumani kupiga hema huko Feisabad, walijikuta kukabiliana na ghasia zilizofanywa na watu wasiopungua 1000, waliowashambulia pamoja na wasaidizi wengine wa kigeni.
Wanajeshi hao wa Ujerumani walirejea nyuma mara moja, hawakutana makabiliano. Alipoulizwa kama wanajeshi wake walijibu barabara ghasia hizo, waziri wa ulinzi wa Ujerumani alijibu kwa ufupi "walizijibu barabara, hatuko hapa kama dola la wakaliaji".
Kuendelea kurundikwa kwa wanajeshi wa Bundeswehr nje ya mji mkuu wa Afghanstan Kabul ni muhimu sana hususan sasa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo tarehe 9 oktoba. Akijibu swali kuhusu ghasia za mara kwa mara dhidi ya wanajeshi wa kusaidia ujenzi upya, waziri Struck alisema:
Inatubidi kumbusha kila mara kwamba, hatuchukui hatua yoyote hapa kama wawakilishi wa polisi wa Afghanistan, hadi pale tu tunapoombwa msaada na maofisa wa serikali, ambao haukuhitajika sana hadi sasa. Mwisho wa kumnukulu waziri wa ulinzi Struck.
Waziri Peter Struck alipata kuijua kambi ya wanajeshi wa Ujerumani iliyoko Kundus alipoitembelea mwezi januari mwaka huu, lakini kambi ya Feisabad ni mpya kabisa kwake, ambamo wanarundikwa sasa wanajeshi wa kusaidia ujenzi upya 110. Licha ya ghasia waziri wa ulinzi anakiri kwamba pia anahangaishwa na jinsi wanajeshi wake wanavyoishi kwa kusongana. Hata hivyo waziri Struck anavutiwa sana na jinsi wanajeshi wake wanavyoshirikiana bega kwa bega na wasaidizi wengine wa misaada ya maendeleo. Wakati jitihada hii ikiendelezwa, vyama vya upinzani vya CDU,CSU na FDP, vinautazama kwa wasiwasi mchango unaotolewa hasa katika Feisabad, kwa sababu, kama vinavyotoa hoja, mchango uliokwishatolewa hadi sasa na shirika la NATO, si wa kuridhisha sana.