Israel Katz atishia kuipoka ardhi ya Wapalestina
21 Machi 2025Katz amesema kwenye taarifa yake kuwa ameliamuru jeshi kuyapoka maeneo zaidi ya Ukanda wa Gaza na kuonya kwamba ardhi kubwa zaidi ya eneo hilo la Wapalestina itachukuliwa na Israel ikiwa Hamas itakataa waachia mateka.
Onyo hilo limetolewa wakati Israel imetanua kampeni yake ya kijeshi iliyoanzisha tena mapema wiki hii na kusambaratisha hali ya utulivu iliyoshuhudiwa tangu kutiwa saini mkataba wa kusitisha vita mwezi Januari.
Soma pia: Israel yatanua kampeni yake ya kijeshi Gaza
Maelfu ya watu walijitokeza wiki hii mjini Jerusalem kupinga kurejea tena kwa mapigano wakimtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kupuuza usalama wa mateka wanaoshikiliwa Gaza.
Wasiwasi huo wa waandamanaji umeoneshwa pia na Rais Isaac Herzog wa Israel aliyesema matendo ya serikali hayawiani na dhamira yake ya kutaka kuwarejesha nyumbani mateka.