Waziri wa Ulinzi Israel aamuru jeshi kuendeleza vita Gaza
1 Juni 2025Hii ni baada ya mjumbe wa Marekani kuliita jibu la karibuni la kundi hilo la wanamgambo kuhusu pendekezo la usitishaji vita huko Gaza kuwa lisilokubalika. Taarifa ya Waziri Katz imesema ni ama Hamas wawaachie mateka, au wataangamizwa.
Wakati huo huo, shambuzulizi la Israel karibu na kituo cha usambazaji misaada huko Gaza limewauwa Wapalestina 31mapema Jumapili. Tukio hilo la mjini Rafah kusini mwa Gaza ni la karibuni katika mfululizo unaodhihirisha ukosefu wa usalama kwenye shughuli za upelekaji wa misaada Gaza, baada ya Israel kupunguza mwezi uliopita mzingiro wake wa ukanda huo, uliodumu kwa takriban miezi mitatu.
Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, lenye uhusiano na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, limesema timu zake za madaktari zimeondoa miili ya Wapalestina 23 na kuwatibu majeruhi wengine 23 karibu na eneo la kusambaza misaada huko Rafah. Maafisa wa afya wa eneo hilo walisema takriban miili 31 ilipelekwa katika Hospitali ya Nasser.
Soma pia: Nchi za Kiarabu zalaani kuzuiwa ziara yao Ukingo wa Magharibi
Jeshi la Israel limesema linachunguza ripoti kwamba Wapalestina walipigwa risasi katika eneo la kusambaza misaada, lakini halijui kuhusu majeraha yaliyosababishwa na ufyatuaji huo wa risasi.