Waziri wa sheria wa DRC akabiliwa na uchunguzi wa ufisadi
30 Mei 2025Bunge la Taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limepitisha azimio la kumruhusu Mwendesha Mashtaka Mkuu kuanzisha uchunguzi dhidi ya waziri wa sheria, Constant Mutamba, ambaye anatuhumiwa kutumia vibaya karibu dola milioni 20 kutoka kwenye mfuko wa fidia kwa waathirika wa vita.
Mutamba, mwenye umri wa miaka 37, aliteuliwa waziri Mei 2024 na amekuwa maarufu kwa matamshi ya kuchochea dhidi ya ufisadi, na aliwahi kupendekeza adhabu ya kifo kwa wanaofuja fedha za umma. Lakini sasa, yeye mwenyewe anakumbwa na tuhuma hizo.
Mutamba anakabiliwa na tuhuma za kutoa zabuni yenye thamani ya dola milioni 40 kwa kampuni ya kizalendo, Zion Construction SARL, ili kujenga gereza karibu na mji wa Kisangani. Ripoti ya kamati maalum ya Bunge imeeleza kuwa zabuni hiyo ilikiuka sheria za manunuzi ya umma, kwani kampuni hiyo ilianzishwa Machi 2024, na haina wafanyakazi waliobobea wala uwezo wa kutekeleza mradi wa aina hiyo.
Inadaiwa kuwa Mutamba alitoa karibu nusu ya bajeti ya mradi huo — sawa na dola milioni 20 — bila kibali cha Waziri Mkuu. Mbaya zaidi, fedha hizo zilitolewa kutoka mfuko wa fidia uliolipwa na Uganda kwa ajili ya waathirika wa vita vya mwaka 2000 kati ya majeshi ya Uganda na Rwanda ndani ya ardhi ya Congo.
Anakana ufisadi, adai kuwindwa kutokana na msimamo wake
Katika video ya TikTok iliyosambaa Jumatatu, Mutamba alimshambulia hadharani Mwendesha Mashtaka Mkuu, Firmin Mvonde, akimtuhumu kuwa sehemu ya "mafia" inayolenga kumvunjia heshima. Alidai pia kuwa anashambuliwa kwa sababu ya msimamo wake dhidi ya rais wa zamani, Joseph Kabila, ambaye anakabiliwa na tuhuma za uhaini kwa madai ya kushirikiana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Licha ya kukiri "makosa ya kiutawala” katika mchakato wa zabuni hiyo, Mutamba amekanusha kufaidika binafsi, akieleza kuwa yote ni "kampeni ya upotoshaji na propaganda juu ya ufisadi wa kufikirika.”
Spika wa Bunge, Vital Kamerhe, alitangaza uamuzi wa kuruhusu uchunguzi huo kupitia matangazo ya televisheni ya taifa, akisema: "Bunge limeridhia kwa kauli moja azimio la kuruhusu uchunguzi dhidi ya Mheshimiwa Constant Mutamba.”
Uamuzi huo ni hatua ya awali. Endapo ushahidi wa kutosha utapatikana, Bunge litapiga kura tena ili kuondoa kinga ya bunge inayomlinda Mutamba, jambo ambalo litamfungulia mlango wa kushitakiwa rasmi mahakamani.
Kwa mujibu wa Transparency International, DRC ni miongoni mwa nchi zilizoathirika sana na ufisadi duniani. Suala hili la Mutamba linaibua tena maswali juu ya dhamira ya kisiasa kupambana na ufisadi, hasa miongoni mwa wale wanaotoa matamko makali ya uwajibikaji huku wakituhumiwa kufanya kinyume.
Iwapo uchunguzi huu utaenda mbele, utakuwa mtihani mkubwa kwa taasisi za sheria za DRC, na jaribio la kuthibitisha kuwa hakuna aliye juu ya sheria — hata wale wanaojitaja kuwa mashujaa wa mapambano dhidi ya ufisadi.