Wadephul: Muhimu kusitishwa mapigano Ukraine
17 Agosti 2025.Akizungumza na kituo cha televisheni cha umma cha Ujerumani ARD, Wadephul amesema kusitisha uhasama ni sharti la awali kwa mazungumzo yoyote ya ziada. Na kuongeza kuwa "bila kusitisha mapigano, si jambo la busara kutarajia mtu yeyote hasa Ukraine, ambayo imevamiwa kuendelea na mazungumzo au kushiriki katika mchakato wa amani.”Kabla ya mkutano huo, Trump alikuwa amesisitiza kusitisha mapigano mara moja, lakini suala hilo halikutajwa katika taarifa zilizotolewa baada ya mkutano. Washirika wa Ulaya walikuwa wamebainisha kusitisha mapigano kama moja ya vipaumbele vyao muhimu kuelekea mazungumzo hayo.Hata hivyo, Wadephul amesisitiza kuwa hakuna mazungumzo yasiyo na maana. Mazungumzo yoyote yanayolenga kumaliza vita ni mazungumzo mazuri na wanayayaunga mkono. Alibainisha kuwa Trump sasa analenga makubaliano ya kina, lakini akasisitiza: "Hakutakuwa na makubaliano kuhusu Ukraine bila Ukraine kuhusishwa."