Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ziarani nchini Urusi
31 Julai 2025Hii ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa serikali mpya ya Syria tangu kupinduliwa mwezi Desemba mwaka jana kwa mshirika wa muda mrefu wa Urusi Bashar al-Assad. Al-Shibani amesema Syria inalenga kurekebisha uhusiano wake na Urusi na kwamba wangependelea kuiona Urusi ikiwa upande wao:
"Syria inatazamia kuwa na ushirikiano kamili na wa kweli na Urusi katika kuunga mkono mchakato wa haki na wa mpito Syria. Hili linaweza kuwa msingi wa ujenzi wa taifa linalotawaliwa kisheria, kuhakikisha kutorudiwa kwa ukiukaji, na kurejesha heshima kwa waathirika."
Kwa upande wake Lavrov amesema Moscow inatumai kuwa Syria itashinda changamoto zote zilizopo na itafanikiwa kurejesha hali ya utulivu na ustawi, na kwamba anatarajia kuwa Rais mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa atahudhuria mkutano wa kilele kati ya Urusi na Jumuiya ya nchi za Kiarabu utakaofanyika mjini Moscow mwezi Oktoba mwaka huu.