Gideon Saar: Israel ni "kiungo muhimu" kwa Ulaya
25 Februari 2025Kauli yake ameitoa wakati Israel imeanza tena mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusu mustakabali wa Gaza iliyoharibiwa na vita.
Saar amefanya mazungumzo na maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels huku EU ikitafakari kuchukua jukumu katika ujenzi mpya wa Gaza baada ya makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano mwezi uliopita.
Soma pia: Israel yasema itachelewesha zoezi la kuwaachia wafungwa wa Kipalestina
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Israel ameshiriki mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel akiwa pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa EU Kaja Kallas, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika tangu mwaka 2022.
Kallas amesema kikao hicho kilikuwa cha "wazi”, akiuambia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari kwamba, amefurahi kushiriki.
Kallas: EU ina wasiwasi kuhusu hali ya Gaza
Mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali katika ukanda wa Gaza na eneo la Ukingo wa Magharibi.
Amesema, "Tumekuwa tukitoa miito kwa pande zote, ikiwa ni pamoja na Israel, kuheshimu sheria za kimataifa za binadamu.”
Ameongeza kuwa, Ulaya haiwezi kuficha wasiwasi wao linapokuja suala la kinachoendelea katika Ukingo wa Magharibi na kwamba wanaunga mkono kurejea nyumbani kwa Wapalestina waliopoteza makaazi yao huko Gaza.
Soma pia: UN yafadhaishwa na ongezeko la machafuko Ukingo wa Magharibi
Kallas amesema pia ni muhimu mpango wa usitishaji mapigano upige hatua kuelekea awamu ya pili na kwamba Umoja wa Ulaya utaunga mkono ujenzi mpya wa ukanda wa Gaza wakati utakapofika.
Shambulio la Hamas katika ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7 mwaka 2023 na jibu la Israel kufuatia shambulio hilo, lilizua mgawanyiko mkubwa ndani ya Ulaya.
Ingawa nchi zote wanachama za Umoja huo zililaani shambulio hilo la Hamas, baadhi zilitetea oparesheni ya kijeshi ya Israel ndani ya Gaza japo wengine walikosoa nguvu kubwa ya kijeshi iliyotumiwa na Israel hasa athari zake kwa raia wa kawaida.
Merz amwalika Netanyahu Ujerumani licha ya hati ya kukamatwa na ICC
Wakati hayo yakiripotiwa, Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz amemwalika Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuitembelea Ujerumani.
Merz amesema atatafuta njia ila kuhakikisha kuwa kiongozi huyo wa Israel hatakamatwa kufuatia hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.
Merz ameuambia mkutano wa waandishi wa habari, siku moja baada ya chama chake cha kihafidhina kushinda katika uchaguzi wa bunge kwamba, ni fikra isiyo na mantiki kwamba Waziri Mkuu wa Israel hawezi kuitembelea Ujerumani.
Soma pia: Viongozi duniani wampongeza Merz kwa ushindi
Mahakama ya Kimataifa ya ICC yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu, Waziri wake wa zamani wa ulinzi pamoja na maafisa wa Hamas kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa kivita uliofanyika Gaza.
Nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya, ikiwemo Ujerumani, ni wanachama wa ICC, ambayo ni mahakama pekee ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Israel hata hivyo inapinga mamlaka ya mahakama hiyo na imekanusha pia madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita.