Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus ahitimisha ziara Tanzania
10 Julai 2025Hii ni baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali akiwamo waziri wa mambo ya nje wa Tanzania.
Miongoni mwa mambo waliyojadiliana ni pamoja suala ya uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba na namna pande hizo mbili zinavyoweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Mwanadiplomasia huyo wa Cyprus ambaye anahitimisha ziara yake ikiwa pia amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa asasi za kiraia na viongozi wa biashara, ziara yake imeangazia kwa kina namna pande hizo zinavyoweza kuudumisha uhusiano wa kiuchumi hasa wakati huu ambako pande hizo mbili zinaadhimisha miaka 50 tangu zilipoasisi mahusiano ya kidiplomasia.
Akizungumza wakati alipomaliza kukutana na mwenyeji wake, waziri wa mashauri ya kigeni wa Tanzania, Mahmud Thabit Kombo, mjumbe huyo wa Umoja wa Ulaya alisema jukumu kubwa la pande hizo mbili ni kuendelea kufungua fursa mpya zitakazowanufaisha wananchi wa Tanzania na washirika wa Ulaya.
Alisema Tanzania ni mshirika wa kuaminika na aliye thabiti katika eneo lenye umuhimu mkubwa.
"Tanzania ni mshirika muhimu katika eneo la kimkakati. Iko imara na yenye amani. Ina uchumi imara na ongezeko nzuri la watu katika eneo linalokabiliwa na changamoto nyingi. Kwa umoja wa ulaya, Tanzania inaweza kuwa eneo letu la kimkakati kwa sera yetu ya mambo ya nje."
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba wajadiliwa
Kiongozi huyo wa Ulaya amejadiliana pia na wenyeji wake kuhusu uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka na ambao joto lake limeanza kushuhudiwa kwa baadhi ya vyama vya siasa vinavyoendesha mchujo kwa wagombea wake.
Suala la amani katika eneo la maziwa makuu limejitokeza pia wakati wa ziara yake hiyo ambayo pia amegusia haja ya pande hizo mbili kuongeza fursa za uwekezaji katika malighafi muhimu na mabadiliko ya kidijitali.
Ziara yake hiyo inakuja wakati pande hizo mbili zikisherekea kutimia miaka 50 tangu kuanzishwa mahusiano ya kidiplomasia, mahusiano ambayo pia yamezidisha msukumu wa shughuli za kimaendeleo.
Kuhusu hatua hiyo, mchambuzi wa masuala ya kidiploimasia na uhusiano wa kimataifa, Dennis Konga anasema Tanzania inaendelea kusalia kama jukwaa la kimkakati kwa jumuiya ya kimataifa kutokana na namna ilivyojiweka kijiografia.
Ziara ya mwanadiplomasia huyo inafuatia mikutano ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Kombo, iliyofanyika Brussels, Ubelgiji mnamo mwezi Aprili na mwakilishi mkuu wa Umoja wa Ulaya, wa Mambo ya Nje na Usalama Kaja Kallas, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa Koen Doens na Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Thomas Östros.