Waziri wa kigeni wa Russia ziarani Berlin
6 Aprili 2006Majadiliano yao yaliofanywa siku ya Jumatano na leo Alkhamis yamehusika na mada za hivi sasa kama vile mgogoro kuhusu mradi wa atomiki wa Iran na hali ya mambo nchini Belarus.
Chini ya uongozi wa Kansela Angela Merkel,uhusiano kati ya Moscow na Berlin umekuwa na utata.Msimamo wa serikali ya Moscow kumuunga mkono dikteta Alexander Lukaschenko wa Belarus,unatazamwa kwa jicho la khofu na Kansela Merkel pamoja na serikali yake.Ingawa Merkel hakutamka cho chote alipokutana na waziri wa kigeni wa Russia Sergei Lavrov wakati wa kupigwa picha,hapo kabla lakini,waziri wa kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alimueleza wazi wazi maoni ya Berlin.Waziri Lavrov kwa upande wake alieleza kuwa Belarus na Ukraine zipo katika hali sawa sawa.Amesema hivi:
”Matokeo ya chaguzi za hivi karibuni nchini Belarus na Ukraine ni matakwa ya raia wa nchi hizo zilizo huru.Madola mengine yanapaswa kuheshimu matokeo ya uchaguzi na yatazamwe kama msingi wa uhusiano pamoja na Minsk na Kiev.Mambo ni mazuri,ikiwa msingi wa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi zingine utaheshimiwa.”
Kwa upande mwingine waziri wa kigeni wa Ujerumani,Steinmeier amesema kuwa kuambatana na misingi ya Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya,masuala ya haki za binadamu na demokrasia yanapohusika,hilo tena si jambo la kuingilia mambo ya ndani.Akaeleza hivi:
“Kwa upande mmoja,umemalizika uchaguzi wa nchini Ukraine ambao umetimiza vipimo vya kimataifa na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya. Upande wa pili,kuna matokeo ya uchaguzi nchini Belarus,ambayo hayambatani kabisa kitarakimu.Kwa hali hiyo,kinyume na Lavrov,tunasema kuwa khofu iliyoelezwa wazi wazi,pamoja na maoni na matumaini yaliyotajwa,si kuingilia mambo ya ndani ya Belarus,bali ni matumaini yanayoambatana na vipimo vilivyowekwa pamoja.”
Lakini kuhusu suala la mradi wa kiatomiki wa Iran kulikuwepo maelewano.Waziri Steinmeier amesema pande zote mbili zimetambua kuwa sasa ni wajibu wa Iran kuchukua hatua ya kutekeleza azimio lililopitishwa hivi karibuni na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,kama inavyotakiwa. Iran itoe ishara dhahiri ya kuweza kurejea kwenye utaratibu wa majadiliano.
Kwa upande mwingine mazungumzo ya Lavrov pamoja na waziri wa ulinzi wa Ujerumani Jung,yalihusika na maslahi ya usalama ya pande mbili.Lavrow amesema walizungumzia ushirikiano kati ya Ujerumani na Russia ili kuimarisha hali ya utulivu nchini Afghanistan sawa na kujitahidi pamoja kutenzua mgogoro unaohusika na mradi wa atomiki wa Iran.