Waziri wa Kenya kuishtaki serikali ya Uingereza
30 Julai 2005Nairobi:
Waziri wa Kenya na rafiki mkubwa wa Rais Mwai Kibaki, ambaye amepigwa marufuku kuingia Uingereza, amesema kuwa ataishtaki serikali ya Uingereza kwa kumvunjia heshima yake. Waziri wa Uchukuzi, Christopher Murungaru, amemlaumu vikali adui wake mkubwa, Balozi wa Uingereza aliyestaafu, Edward Clay, ambaye wakati mmoja alimwita kuwa ni Jasusi anayetumia mbinu za kikoloni kuchochea mivutano ya kikabila kwa kuilaumu serikali ya Kenya. Waziri Murungaru amesema kuwa serikali ya Uingereza lazima itoe ushahidi wa makosa yake na ifikirie athari zake kwa sababu ataichukulia hatua kali za kisheria. Ameongeza kusema kuwa atajitetea katika Mahakama ya Nairobi au mahali pengine popote pale. Serikali ya Uingereza, mapema juma hili, imebatilisha viza ya Waziri Murungaru kwa mujibu wa sheria za uhamiaji zinazowazuia waliofanya vitendo vibaya vya jinai na walaji rushwa na magendo kuingia Uingereza.