Waziri mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou aondolewa
9 Septemba 2025Waziri Mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou aliwafumbia macho hata washirika wake kwa kuitisha kura ya imani kuutafutia ufumbuzi mzozo wa muda mrefu kuhusu bajeti yake ya kubana matumizi, ambayo ililenga karibu euro bilioni 44 za kuokoa gharama ili kupunguza mrundikano wa deni la Ufaransa.
Katika kura iliyopigwa katika bunge la Kitaifa, wabunge 364 walipiga kura kuunga mkono hoja kwamba hawana imani na serikali huku, 194 pekee wakisema wana imani nayo. "Kulingana na ibara ya 50 ya katiba, waziri mkuu lazima awasilishe barua ya kujiuzulu kwake," alisema spika wa bunge Yael Braun-Pivet.
Bayrou amekuwa waziri mkuu wa kwanza katika historia ya Ufaransa ya miaka ya karibuni kuondolewa madarakani kwa kura ya imani badala ya kura ya kutokuwa na imani naye.
Ofisi ya rais wa Ufaransa ilisema katika taarifa yake kwamba rais Emmanuel Macron "amezingatia" matokeo na kusema atamtaja waziri mkuu mpya "katika siku zijazo", na kufikisha mwisho uvumi uliobaki kwamba rais badala yake anaweza kuitisha uchaguzi wa mapema.
Macron atakutana na Bayrou Jumanne "kukubali kujiuzulu kwa serikali yake", iliongeza.
Bayrou ni waziri mkuu wa sita chini ya Macron tangu kuchaguliwa kwake mnamo mwaka 2017 lakini wa tano tangu 2022. Kuondolewa kwa Bayrou kunamwacha mkuu huyo wa taifa la Ufaransa na mtihani mpya wa ndani ya nchi unaomumiza kichwa katika wakati anapoongoza juhudi za kidiplomasia kuhusu vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Lakini akitetea uamuzi wake wa kuitisha kura hiyo ya imani yenye hatari kubwa, Bayrou aliliambia Bunge la Kitaifa: "Hatari kubwa ilikuwa ni kutochukua hatua moja ya hatari, na kuwacha mambo yaendelee bila mabadiliko yoyote... na kufanya shughuli kama kawaida."
Akielezea mrundikano wa deni kama "wa kutishia maisha" kwa Ufaransa, Bayrou alisema serikali yake ilikuwa imeweka mpango ili nchi hiyo "katika muda wa miaka michache iepuke wimbi lisiloweza kuepukika la deni ambalo linaizamisha".
Rais asiyependwa
Macron sasa anakabiliwa na moja ya maamuzi muhimu zaidi ya urais wake juu ya nani wa kumteua kama waziri mkuu wa saba wa mamlaka ambayo yanazidi kuwa magumu.
Chama cha Kisoshalisti (PS) kimeelezea utayarifu wa kuongoza serikali mpya lakini haijafahamika ikiwa utawala kama huo unaoongozwa na mwanasiasa kama vile kiongozi wa chama hicho Olivier Faure unaweza kudumu.
"Nadhani ni wakati wa mrengo wa kushoto kutawala nchi hii tena na kuhakikisha kuwa tunaweza kuvunja sera za miaka minane iliyopita," Faure aliiambia televisheni ya TF1.
Mawaziri vigogo wa baraza la mawaziri wa vyama vya mrengo wa kulia, kama vile Waziri wa Sheria Gerald Darmanin, wanaaminiwa na Macron lakini wana hatari ya kupigiwa kura na kutolewa na wabunge wa vyama vya mrengo wa kushoto.
Wanasiasa wahaiba ya chini ambao wanaweza kupata maafikiano ya wanasiasa wa vyama vya mrengo wa kati na kushoto ni pamoja na Waziri wa Afya Catherine Vautrin katherin votraa au Waziri wa Fedha Eric Lombard.
Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na shirika la Odoxa-Backbone kwa ajili ya gazeti la Le Figaro, asilimia 64 ya Wafaransa wanataka Macron ajiuzulu badala ya kutaja waziri mkuu mpya, hatua ambayo ameifutilia mbali. Haruhusiwi kugombea muhula wa tatu mnamo 2027.
Le Pen akitawala
Kando na msukosuko wa kisiasa, Ufaransa pia inakabiliwa na mivutano ya kijamii. Kundi la siasa za mrengo wa kushoto linaloitwa "Block Everything" - "Zuia Kila Kitu" limeitisha siku ya kuchukua hatua Jumatano, na vyama vya wafanyikazi vimewataka wafanyikazi kugoma mnamo Septemba 18.
Uchaguzi wa urais wa 2027 wakati huo huo bado upo wazi, huku wachambuzi wakitabiri kuwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Ufaransa kitakuwa na nafasi bora zaidi kuwahi kuwa nayo, ya kushinda.
Mgombea mara tatu wa urais kwa tiketi ya National Rally (RN) Marine Le Pen alipata pigo mwezi Machi wakati mahakama ya Ufaransa ilipomtia hatiani yeye na maafisa wengine wa chama kutokana na kashfa ya kughushi ya ajira katika bunge la Umoja wa Ulaya.
Le Pen alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela, miwili kati yake ilisitishwa, na pia kumpiga marufuku kugombea nafasi hiyo kwa miaka mitano, jambo ambalo litazuia azma yake ya kushiriki katika uchaguzi wa 2027 -- isipokuwa kama hukumu hiyo itaibatilishwa kwa kukata rufaa.
Lakini mahakama ya mjini Paris ilisema Jumatatu rufaa yake itasikilizwa kuanzia Januari 13 hadi Februari 12, 2026, kabla ya uchaguzi huo -- hali inayoleta uwezekano wa kufufua matumaini yake ya kuwania urais wa Ufaransa.
Akishangiliwa na wabunge wake, Le Pen alimtaka Macron kuitisha uchaguzi wa mapema wa wabunge, akisema kufanya uchaguzi "sio chaguo bali ni wajibu".