Mkuu wa Wahouthi Yemen auawa katika shambulizi la Israel
31 Agosti 2025Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Wahouthi, Mahdi al-Mashat, alithibitisha tukio hilo, akisema watu wengine pia walijeruhiwa. Israel imesema shambulizi hilo lililenga maafisa wakuu akiwemo mkuu wa utumishi wa serikali na waziri wa ulinzi, ingawa haijathibitishwa iwapo waziri huyo ameuawa. Naibu waziri mkuu, Mohammed Miftah, amepewa jukumu la kuongoza serikali kwa sasa.
Rahwi, aliyeteuliwa mwaka uliopita, alionekana kama kiongozi wa heshima bila ushawishi mkubwa, huku nguvu halisi zikibaki mikononi mwa viongozi wa ndani wa kundi hilo. Yemen imegawanyika tangu 2014 kati ya utawala wa Wahouthi huko Sanaa na serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia mjini Aden.
Shambulizi hili linakuja wakati mvutano kati ya Israel na Wahouthi ukiongezeka tangu kuanza kwa vita vya Gaza mwaka 2023, ambapo Wahouthi wamekuwa wakishambulia meli katika Bahari ya Shamu na kurusha makombora kuelekea Israel, mengi yakiwa yamezuiwa. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema shambulizi hilo ni "pigo kubwa” kwa Wahouthi na kwamba "huo ni mwanzo tu,” huku Wahouthi wakiahidi kulipiza kisasi.