Waziri Mkuu wa Nepal ajiuzulu kufuatia maandamano ya Umma
9 Septemba 2025Uamuzi huo ambao haukutarajiwa umetangazwa na ofisi ya waziri mkuu Khadga Prasad Oli saa chache baada ya maandamano makubwa ya vijana yaliyoshuhudiwa kwenye miji mbalimbali ya taifa hilo kugeuka ya vurugu.
Tangazo la kujiuzulu kiongozi huyo lilipokelewa kwa furaha na maelfu ya waandamanaji waliokusanyika katikati mwa mji mkuu Kathmandu. Kipande kimoja cha video kimemwonesha mwandamanaji akimkumbatia mwenziwe na kumwambia "tumeshinda" baada ya kutolewa taarifa kujiuzulu waziri mkuu.
Taarifa za kung´atuka kwa Oli zimetolewa ikiwa ni saa chache tangu makundi ya vijana wenye hasira walipoyavamia majengo ya serikali ikiwa ni pamoja na nyumba ya kiongozi huyo, mawaziri na hata bunge wakayachoma moto au kufanya uharibifu mkubwa.
Msaidizi wa waziri mkuu Oli amesema nyumba binafsi ya kiongozi huyo ilivamiwa na waandamanaji waliovunja madirisha, vyombo, viti na samani nyingine kabla ya kuitia moto. Jengo pia la Bunge la Taifa kwenye mji mkuu, Kathmandu lilishambuliwa na sehemu yake kuchomwa moto.
Vijana wapinga ufisadi na kufungiwa mitandao ya kijamii
Vijana hao wameghadhabishwa na uamuzi wa hivi majuzi wa serikali wa kuifunga mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Tiktok, X na Instagram. Mitandao mikubwa ya kijamii ilifungwa ili kuishinikiza kutekeleza masharti ya serikali iikiwa ni pamoja na kuteua mwakilishi atakaewajibika kwa niaba ya kampuni zinazoendesha mitandao hiyo.
Wakosoaji wa uamuzi huo wa serikali wanasema hatua hiyo ililenga kuzuia utoaji maoni na kuwaandamiza wapinzani wanaitumia mitandao kuinyooshea kidole serikali. Hata hivyo baadhi ya vijana walioingia mitaani wanasema maandamano hayo ni zaidi ya uamuzi wa kufungiwa mitandao ya kijamii. Safal Andolankari ni mmoja waliondamana mjini Kathmandu.
"Kwanini kuna hasira kubwa hivi? Vyombo vya kimataifa vinaamini hili limetokea kwa sababu mitandao imezuiwa. Hapana, hizi ni hasira zilizokaa vifuani kwa zaidi ya miongo miwili, zikichochewa na ufisadi. Na kila mtu amechoka. Hawa majambazi wametutesa kwa muda mrefu, na unachokiona ni cheche tu iliyowashwa na mitandao ya kijamii"
Serikali ya Waziri Mkuu Oli ilichukua hatua ya kuufuta uamuzi wake wa kuifunga mitandao ya kijamii lakini maandamano ya umma yaliendelea kutwa nzima hii leo yakigeuka kuwa dhidi ya ukandamizaji wa polisi na tuhuma za rushwa na ufisadi serikalini.
Oli, mwanasiasa wa kikomunisti aliingia madarakani mwaka mmoja uliopita akihaidi uthabiti na kubuni nafasi nyingi za ajira baada ya miongo kadhaa ya misukosuko iliyoliandama taifa hilo la safu za milima ya Himalaya.
Alipoapishwa mwezi Julai mwaka jana, ilikuwa ni mara yake ya nne kuchukua wadhifa wa uwaziri mkuu na alitoa matumaini ya kupambana na rushwa, umasikini na kukomesha ukandamizaji wa muda mrefu nchini Nepal.
Pamoja na ahadi zote hizo mwaka mmoja baadae vijana bado wanalalamikia ukosefu wa nafasi za kazi na madai ya upendeleo serikalini. Ukosefu wa ajira nchini Nepal ulifikia asilimia 20 mwaka uliopita, takwimu hizo ni kulingana na Benki ya Dunia.
Katika juhudi za kutuliza hali ya mambo, Rais Ramchandra Paudel wa nchi hiyo ameahidi kukutana na makundi ya vijana wiki inayokuja. Pia ametoa mwito wa mshikamano wa taifa akiwarai vijana kutumia njia za amani kutafuta suluhu kwa mzozo unaoikabili Nepal.