Waziri mkuu Jaafari anamatumaini juu ya katiba mpya ya Iraq
23 Agosti 2005Matangazo
Baghdad:
Waziri mkuu wa Irak Ibrahim Jaafari amesema ana yakini makubaliano yatafikiwa juu ya katiba mpya ya nchi hiyo. Bw Jaafari alisema masuala mengi yameshatatuliwa, ikiwa ni pamoja na suala kuu kuhusu mfumo wa Shirikisho. Matamshi yake yamekuja siku moja baada ya maafisa wa Kikurdi na Shia kuwasilisha mswaada rasmi wa katiba bungeni. Hata hivyo kura iliotazamiwa kupigwa bungeni imecheleweshwa hadi tafauti zilizosalia zimesuluhishwa.
Ingawa Washia na Wakurdi wana kura zinazotosha kushinikiza mswaada huo kupita , maafisa wa Kisunni wameonya kwamba kupitishwa kwake kunaweza kuzusha vita vya kiraia. Wanasiasa wa Kisunni wanapinga mfumo wa Shirikisho wakisema utaigawa Iraq.