Waziri Israel asema ni wakati wa kutumia nguvu kamili Gaza
30 Mei 2025Hii ni baada ya Hamas kusema kuwa pendekezo jipya la amani la Marekani, halikuyafikia matakwa yake.
Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, Ben Gvir amesema kwa sasa hakuna kisingizio tena.
Ikulu ya White House jana ilisema Rais Donald Trump na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff waliwasilisha pendekezo la amani kwa Hamas, ambalo liliungwa mkono na Israel.
Israel lakini haijathibitisha iwapo imeliidhinisha hilo pendekezo jipya la usitishaji mapigano la Marekani.
Wakati huo huo Ufaransa imetangaza kwamba huenda ikawa na msimamo mkali kwa Israel iwapo itaendelea kuzuia misaada ya kiutu kuingia Gaza.
Haya yamesemwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
"Naamini kuwa kila kitu kitategemea maamuzi yatakayofanywa na serikali ya Israel katika siku zijazo. Na ni wazi leo kwamba hatuwezi kuiwacha hali hii kuendelea kwasababu kuzuiwa kwa misaada kunasababisha hali mbaya. Wiki chache zilizopita niliweza kwenda katika eneo la mpakani na Rais Sisi wa Misri, niliona hali ya kukata tamaa ya waliojeruhiwa waliokuwa wakitibiwa katika hospitali za Misri, majeruhi waliofanikiwa kukimbia wakati kulipokuwa na usitishwaji wa wiki kadhaa wa mapigano," alisema Macron.
Macron yuko Singapore kwa ziara rasmi.