Waziri atetea kukamatwa kwa Mtangazaji Uganda
14 Agosti 2005Kampala:
Waziri wa Habari wa Uganda, Nsaba Buturo, leo ametetea kukamatwa juma lililopita Mtangazaji wa Redio aliyezungumzia kifo cha Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang. Bw. Buturo amesema kuwa usemi wa Mtangazaji huyo ungalisababisha mauaji ya halaiki. Waziri Buturo amesema kuwa usemi wa Mtangazaji Andrew Mwenda, ambaye amekamatwa kwa tuhuma za uchochezi, umehatarisha amani ya taifa na kimkoa kwa kutangaza uchochezi kuhusu kifo cha hayati Garang. Bw. Buturo amesema kuwa maneno ya uchochezi ya Bw. Mwenda yametolewa wakati ambapo kulikuwa na mivutano mikali ndani ya Sudan ambako tayari watu wapatao zaidi ya 100 wameuawa. Waziri Buturo amesema kuwa kila mtu anakumbuka kile kilichotokea Rwanda mwaka 1994 ambacho kimechochewa na matangazo ya Radio Mille Collines. Redio ya kibinafsi ya KFM ambayo imetangaza habari hizo nayo pia imefungwa. Hatua hiyo imelaumiwa vikali ndani na nje ya Uganda kuwa inakwenda kinyume na uhuru wa vyombo vya habari.