Palestina yaishutumu Israel kutaka kukiangamiza kizazi chao
28 Aprili 2025Balozi wa Palestina nchini Uholanzi, Ammar Hijazi, ameiambia hayo Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ya mjini The Hague wakati mahakama hiyo ikianza kusikiliza madai kuhusiana na wajibu wa Israel katika kuhakikisha na kuwezesha uingizwaji wa msaada wa kibinadamu unaohitajika haraka kwa raia wa Palestina.
Alisema "Ninapowahutubia leo, watu wa Palestina wanakufa kwa njaa, wanapigwa mabomu na kuhamishwa kwa nguvu na Israel. Israel haijaruhusu chakula, maji, dawa na vifaa vya matibabu au mafuta kuingia Gaza kwa muda wa miezi miwili iliyopita - sera inayoungwa mkono na mahakama ya juu zaidi nchini Israel ambayo mara kadhaa ilikataa maombi ya kuruhusu msaada Gaza. Kifo kinawanyemelea kwa kiasi kikubwa."
Hijazi aidha ameelezea mazingira yasiyovumilika yanayowakabili wakazi wa Gaza tangu kuzuiwa kwa misaada ya kibinadamu Machi 2 na kuongeza kuwa Gaza inageuka kuwa "kaburi la halaiki kwa watu wa Palestina na wale waliokwenda kuwasaidia.