Wawakilishi wa mataifa 40 wakutana London kujadili uhamiaji
31 Machi 2025Kwenye ufunguzi rasmi wa kongamano hilo la kihistoria, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, aliyatolea wito mataifa kuungana na kutumia rasilimali kwa pamoja kupambana na uhamiaji haramu katika kila hatua kutokea kaskazini mwa Afrika, Mashariki ya Kati hadi Uingereza.
''Uhamiaji haramu unachangia pakubwa katika ukosefu wa usalama duniani. Unatunyima uwezo wetu wa kudhibiti wanaoingia humu. Na hilo linawakasirisha wengi. Binafsi linanikera. Tutafanikiwa kuyavunja magenge haya ikiwa tutashirikiana. Hatuna jinsi ila kulikabili moja kwa moja,'' alisema Starmer.
Uingereza mwenyeji wa mkutano wa 'biashara chafu' ya wahamiaji
Wawakilishi hao wa mataifa zaidi ya 40 ni pamoja na Marekani, Vietnam, Iraq na Ufaransa waliokuja pamoja kusaka mbinu mpya ya kuyavunja magenge haramu ya kusafirisha binadamu na kuimarisha usalama mipakani. Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano wa kimataifa kujadili vyanzo vya uhamiaji haramu kutokea magenge ya halifu, ufadhili haramu hadi matangazo kwenye mitandao ya kijamii.
Kikao hicho kinawajumuisha pia wawakilishi wa makampuni ya mitandao ya kijamii ya Meta, X na TikTok kuzungumzia njia za kushirikiana kuupiga vita mitandaoni uhamiaji haramu. Ili kuwasili Uingereza, duru zinaeleza kuwa wahamiaji huwalipa wasafirishaji haramu maelfu ya paundi za Uingereza ili kuvukishwa kwenye ukanda ulio na biashara kubwa za baharini ili kutua kwenye maeneo ya pwani.
Ni muhimu kushirikiana kuupiga vita uhamiaji haramu
Waziri wa Usalama wa Uingereza, Yvette Cooper, anausisitizia umuhimu wa kushirikiana kuupiga vita uhamiaji haramu.
''Tunafahamu kuwa kuimarisha usalama kwenye mipaka yetu ina maana ya kufanya kazi na mataifa yaliyoko upande wa pili wa mipaka na wala sio kupiga kelele kwenye pwani zetu. Tunajua fika kwamba hakuna nchi inayoweza kufanikiwa peke yake. Hii ndio maana ushirikiano na wote walioko hapa una umuhimu mkubwa,'' aliongeza kusema Yvette Cooper.
Umoja wa Ulaya kupendekeza kanuni kali kuwaondoa wahamiaji
Ifahamike kuwa mpango wa kuwarejesha wahamiaji Rwanda uliotangazwa mwaka 2022 na serikali iliyopita ya Rishi Sunak ulikumbwa na matatizo ya kisheria. Kwa upande wa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ameitetea serikali yake kuwa imefanikiwa kuwarejesha zaidi ya wahamiaji alfu 24 tangu aingie madarakani, idadi ambayo ni kubwa zaidi katika kipindi cha miaka minane iliyopita.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani anayemaliza muda wake, Nancy Faeser amewatolea wito washirika wa Ulaya kubadilishana maelezo na kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuimaliza nguvu mifumo haramu ya kusafirisha binadamu na magenge ya wahalifu hao kwa jumla.