Waislamu washerehekea siku kuu ya Eid ul Fitr
31 Machi 2025Waumini wa dini ya Kiislamu walimiminika katika misikiti kote nchini Kenya na viwanja mbali mbali kwa ibada ya maombi kabla ya kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki kwa sherehe za Eid ul Fitr. Mfungo wa Ramadhan ulikamilika rasmi baada ya kuandama kwa mwezi kuashiria kuwa waislamu walifunga kwa siku 29 mwaka huu. Ali Hassan Joho, Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini amewarai wakenya kuiunga serikali mkono.
“Tuiunge serikali mkono, ndio ile siasa ya kufa kupona, watu wanashindana kish awa pili kwa urais anapoteza kila kitu, kwa hivyo tuwaunganishe Wakenya,” alisema Waziri Joho.
Wapalestina waadhimisha Eid kwa mashambulizi makali kutoka Israel
Mfungo wa Ramadhan ni mojawapo ya nguzo tano kuu za Uislamu, ambapo Waislamu hufunga kula na kunywa huku wakiomba. Sherehe hizi hujumuisha mlo wa pamoja, wakati familia na marafiki wanapokutana ili kusherehekea na kufurahia matunda ya ibada zao. Wengi hujitoa kwa kutoa misaada kwa wenye uhitaji, kuonyesha roho ya ukarimu na mshikamano ndani ya jamii.
Salim Mvurya ni Waziri wa Biashara na Uwekezaji, amesisitiza kwamba“Sherehe za Eid ziendane kulingana na dini ya kiislamu na kutoa wito pia wa watu walionacho kuendelea kuwajali wasiojiweza katika jamii.
Viongozi wasisitiza umoja wa kijamii na mshikamano
Inspekta Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, aliungana na waumini, akiwemo Mbunge wa Kamukunji Yusuf Hassan, kwa ajili ya sala na sherehe za Eid-ul-Fitr katika mtaa wa Eastleigh hapa Nairobi akitoa hakikisho kuhusu usalama wa taifa.
“Ombi langu ni moja, tuendelee kushirikiana na kutangamana pamoja, tunawashukuru watu wanaokaa hapa maana wanashirikiana na polisi kuhakikisha watu wanakaa kwa amani,” alisisitiza Inspekta Douglas Kanja.
Waislamu Uganda waadhimisha Eid-ul-Fitr wakilaani vita vya Sudan
Nchini Kenya sherehe hizo zilianza kuadhimishwa siku ya Jumapili huku serikali ikitangaza leo Jumatatu (31.03.2025), kuwa siku ya likizo kuruhusu waislamu kuhitimisha mwezi wa funga na kuendelea na sherehe zenyewe. Baadhi ya waumini wamesema kuwa kipindi cha Ramadhani kiliwapa nafasi ya kujitathmini, kuimarisha imani yao, na kujenga mahusiano mema na wengine. Sherehe za Eid ul-Fitr ziliwapa fursa ya kusherehekea mafanikio hayo na kuanza upya kwa ari na nguvu mpya.
Sherehe za Idd ul-Fitr nchini Kenya zilifanyika kwa amani zikionyesha uzito wa umoja wa kijamii na umuhimu wa maadili katika kujenga taifa lenye mshikamano na maendeleo. Hapa DW, tunawaambia waislamu wote Idd Muburak.
Shisia Wasilwa, DW Nairobi.