Watu 30 wauawa, 80 wajeruhiwa kufuatia shambulio la Urusi
13 Aprili 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amelaani shambulio hilo akilitaja kuwa moja ya mashambulizi mabaya zaidi dhidi ya Ukraine kwa mwaka huu na kutoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kali dhidi ya Moscow.
Kupitia mitandao ya kijamii Zelensky amesema "watu waovu pekee" ndio wanaoweza kutekeleza aina hiyo ya ukatili dhidi ya raia, huku akiambatanisha video ilionesha miili ya watu iliyotapakaa barabarani, magari na miundombinu iliyoharibiwa baada ya shambulio hilo.
Soma pia: Urusi yafanya mashambulizi ya droni 88 dhidi ya Ukraine
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine imesema wengi wa wahanga wa shambulio hilo walikuwa barabarani, kwenye magari ikiwemo usafiri wa umma shambulio hilo lilipotokea.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Antonio Costa kupitia mtandao wa kijamii wa X, amelaani hatua hiyo ya Urusi na kuongeza kuwa shambulio hilo la 'umwagaji damu' linaashiria kuwa Moscow inachochea kuendelea kwa vita hivyo.