Watu zaidi ya 1,000 wakamatwa katika maandamano ya Urusi
23 Januari 2021Mjini Moscow, karibu waandamanaji 5,000 waliujaza uwanja wa Pushkin katikati mwa mji huo mkuu, ambako makabiliano yalizuka na waandamanaji wakaburuzwa na askari wa kutuliza na ghasia hadi kwenye mabasi ya polisi na kuzuiliwa kwenye malori.
Mke wa Navalny, Yulia Navalnaya ni miongoni mwa waliokamatwa. Maandamano hayo yalishuhudiwa katika maeneo mengi ya Urusi kuanzia mji wa kisiwa wa Yuzhno-Sakhalinsk kaskazini mwa Japan na mji wa mashariki mwa Siberia wa Yakutsk ambako baridi kali limetanda, mpaka miji mingine ya Urusi yenye watu wengi katika upande wa Ulaya. Ukubwa huo wa maandamano unaashiria jinsi Navalny na kampeni yake ya kupambana na rushwa walivyojenga mtandao mpana ya uungaji mkono licha ya ukandamizaji rasmi wa serikali na kupuuzwa kila mara ya vyombo vya habari.
Mkosoaji mkubwa wa Putin aliitisha maandamano makubwa mara baada ya kunusurika jaribio la kulishwa sumu ya Novichok na kurejea mjini Moscow wiki iliyopita, kufuatia miezi kadhaa ya kupatiwa matibabu Ujerumani. Alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Sheremetyevo na kufungwa.
Maandamano ya Jumamosi (23.01.2021) yanatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa upinzani katika kuhimiza maandamano licha ya shinikizo kutoka kwa Kremlin dhidi ya wakosoaji wake na janga la virusi vya corona.
Kuelekea maandamano hayo timu ya mwanasiasa huyo wa upinzani ilitoa nyaraka za uchunguzi kuhusiana na mali za kifahari katika bahari nyeusi zinazodaiwa kumilikiwa na Putin. Tangu zitolewe zimetizamwa mara milioni 65. Katika bandari ya Vladivostok waandamanaji walikusanyika katikati ya mji huo, wakipiza sauti za "Putin ni mwizi" na "Uhuru wa Navalny".
Waandamanaji pia walikusanyika katika miji ya Mashariki ya mbali na mkoa wa Siberia ikiwemo Khabarovsk, Novosibirsk na Chita ambako maelfu ya waandamanaji wamejitokeza. Shirika moja la OVD ambalo linafuatilia mikutano ya upinzani limesema kwa kukadiria polisi wamewakamata takribani watu 200 kwenye miji 20.
Polisi mjini Moscow, waliapa kuchukua hatua kali dhidi ya waandamanaji wakisema matukio yote ya umma yaliyopigwa marufuku "yatazuiliwa mara moja." Navalny ambaye anashikiliwa chini ya ulinzi mkali katika jela ya Matrosskaya Tishina mjini Moscow amewashukuru wafuasi wake.
"Nafahamu vyema kabisa kwamba kuna watu wengi wazuri nje ya kuta za jela na usaidizi utakuja", alisema Navalny siku ya Ijumaa. Mke wa kiongozi huyo Yulia, alisema angeungana na waandamanaji mjini Moscow.
Kuelekea maandamano ya Jumamosi, washirika kadhaa wa Navalny akiwemo msemaji wake Kira Yarmysh walikamatwa na polisi kwa kukiuka sheria za kuandamana na kupewa kifungo kifupi jela. Navalny alihukumiwa siku 30 jela siku ya Jumatatu na wafuasi wake wana hofu kwamba mamlaka zinajiandaa kumfunga kwa muda mrefu ili kumnyamazisha. Navalny mwenye umri wa miaka 44 alipata umaarufu muongo mmoja uliopita na tangu wakati huo amekuwa kinara wa harakati za upinzani nchini Urusi na kuongoza maandamano makubwa dhidi ya ufisadi na udanganyifu katika uchaguzi.
Kukamatwa kwake kumelaaniwa na mataifa kadhaa ya magharibi, huku Marekani, Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Canada zikitaka aachiwe huru.