Watu wenye silaha wavamia Tume ya Haki za Binadamu Kenya
6 Julai 2025Shambulio hilo limetokea Jumapili, siku moja kabla ya maadhimisho ya "Saba Saba", siku ya kihistoria inayokumbusha mapambano ya demokrasia nchini humo. Kwa mujibu wa mashuhuda, watu hao wapatao ishirini walivunja lango na kuanza kuwashambulia waliokuwepo, wakidai wanapanga maandamano. Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa kwa ushirikiano na Women's Collective Kenya, kundi la kijamii linalopigania haki za wanawake na vijana waliopotea au kuuawa na polisi. Waliowashambulia walikuwa na silaha kama virungu, huku wengine wakionekana kushirikiana na polisi hali iliyojitokeza pia katika maandamano ya Juni 17, ambapo waandamanaji walivamiwa na wanaume waliokuwa wamepanda pikipiki na kubeba mijeledi. Tangu Juni, takriban watu 19 wameuawa katika maandamano, huku hasira dhidi ya Rais William Ruto zikiongezeka kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.