Watu wengine 23 wauawa Gaza
10 Aprili 2025Ndege za Israel zililishambulia jengo hilo la makazi ya watu katika eneo la Shijaiyah lililopo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya takriban watu hao 23.
Kwa mujibu wa maafisa wa afya katika hospitali ya Al-Ahly wanawake wanane na watoto wanane ni miongoni mwa watu waliouawa. Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas pia imethibitisha takwimu hizo.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema vikosi vya Israel vimechukua eneo la ziada katika Ukanda wa Gaza na ameeleza kwamba maeneo yanayochukuliwa yanaongezwa katika orodha ya sehemu zilizotengwa na serikali ya Israel kwa ajili ya usalama.
Huku Israel ikiongeza shinikizo kwa Hamas ili wakubali kuwaachilia huru mateka, jeshi limetoa maagizo mapya ya watu kuondoka kwenye sehemu za Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na mji wa Shijaiyah.
Israel imezuia kabisa kuingia katika Ukanda wa Gaza chakula, mafuta na misaada mingine ya kibinadamu jambo ambalo limewaacha raia wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya kila siku.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, amesema juhudi za kufikisha misaada kwenye Ukanda wa Gaza zimebanwa kwa kiwango kikubwa na Israel.
Tamko la Macron lapingwa
Huku hayo yakiendelea Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar, amelilaani tamko la Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyesema kwamba nchi yake inaweza kulitambua taifa la Palestina ifikapo mwezi Juni. Katz amesema hatua kama hiyo itakuwa ni kama "kuupa tuzo ugaidi.” Macron amesema Ufaransa inapaswa kupiga hatua kuelekea kulitambua taifa la Palestina katika miezi ijayo wakati Ufaransa na Saudi Arabia zitakapoandaa mkutano wa kimataifa kuhusu utekelezaji wa suluhisho la kuundwa mataifa mawili ya Israel na Palestina.
Soma pia: Mkuu wa UN Guterres asema Gaza imegeuka uwanja ya mauaji
Takriban nchi 150 zinalitambua taifa la Palestina. Mnamo mwezi Mei mwaka uliopita wa 2024, Ireland, Norway na Uhispania zilitangaza kuitambua Palestina, zikifuatiwa na Slovenia mwezi Juni.
Ufaransa itakuwa taifa kubwa la Ulaya kulitambua taifa la Palestina, hatua ambayo Marekani ingawa imekuwa ikipinga kwa muda mrefu, lakini wako baadhi ya wanasiasa wanaoiona kama ni hatua ya lazima itakayoweza kuleta utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Vyanzo: AFP/AP/DPA