Wawili wauwawa katika maandamano ya kupinga serikali, Kenya
25 Juni 2025Maelfu ya wakenya walijitokeza leo katika kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu waandamanaji maarufu Gen Z, walipolivamia bunge la nchi hiyo katika maandamano ya kuipinga serikali ya rais William Ruto.
Polisi iliwarushia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji hao na kuzua vurugu zilizosababisha watu kadhaa kuuwawa na kujeruhiwa huku maandamano hayo yakisambaa katika maeneo mengine ya nchi kama Mombasa, Kisumu, Nakuru na Nyahururu,
Wanaharakati na familia ya waathiriwa waliitisha maandamano ya amani hii leo, kuwakumbuka zaidi ya watu 64 walioangamia mwaka jana na wengine 20 ambao hadi sasa hawajulikani waliko. Hussein Khaled ni mmoja wa wanaharakati hao anaetetea haki za binaadamu.
Balozi za Magharibi zahimiza amani Kenya
"Tuko hapa kudai haki kwa mashujaa wetu. Wakenya 64 waliuawa mwaka jana. Hadi kufikia sasa, hakuna afisa hata mmoja ambaye amechukuliwa hatua. Kwa hivyo tuko hapa leo kudai haki, haki kwa maana ya kulipwa fidia, haki kwa maana ya kukamatwa kwa maafisa waliohusika na mauaji, haki katika suala pia la mageuzi ya katika idara za polisi kwa sababu wakenya wengi wanapoteza maisha mikononi mwao. Kwahiyo tunadai haki kwa kila mtu ndio tuweze kusonga mbele kama taifa," aliendelea kusema HusseinKhalid.
Vijana wa Kenya wamechoshwa na utawala wa rais William Ruto kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha na ukatili wa polisi. Hivi karibuni mwanablogu ambae pia ni mwalimu Albert Ojwang aliuawa akiwa mikononi mwa polisi.