Watu wawili wauawa katika mapigano mapya kusini mwa Syria
3 Agosti 2025Watu wawili wameuawa baada ya mapigano ya kikabila kuibuka tena katika mkoa wa Sweida kusini mwa Syria wenye idadi kubwa ya watu wa jamii ya Druze. Mapigano hayo mapya ni tukio la kwanza la vurugu tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi uliopita.
Shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini humo lenye makao yake makuu Uingereza, Syrian Observatory for Human Rights, limeeleza kuwa mwanachama mmoja wa vikosi vya usalama na mpiganaji wa jamii ya Druze wameuawa huku watu wengine saba wakijeruhiwa baada ya mapigano kuzuka karibu na eneo la Tal Hadid, magharibi mwa mkoa wa Sweida.
Tal Hadid ni "eneo la kimkakati" lililoko kwenye mwinuko na linachukuliwa kuwa muhimu katika usalama kwani yeyote anayelidhibiti anaweza kufuatilia kinachoendelea katika maeneo jirani kwa urahisi.
Mwezi Julai mwaka huu, mkoa wa Sweida kusini mwa Syria ulishuhudia machafuko makubwa ya kikabila na kimadhehebu kati ya wapiganaji wa jamii ya Druze na Waarabu wa Sunii wa jamii ya Wabedui yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu na kuibua mgawanyiko wa kijamii na kisiasa.
Makubaliano ya kusitisha vita yaliweka kikomo umwagaji damu – ambapo zaidi ya watu 1400 waliuawa – kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria – lakini hali inaendelea kuwa tete huku machafuko yakiibuka tena leo.