Watu watano wakutwa na maambukizi ya Ebola Uganda
3 Februari 2025Sambamba na hatua za kuepusha kusambaa kwa ugonjwa huo, maafisa wanaandaa kujaribisha chanjo dhidi ya virusi vya ebola ambapo dozi 2,000 zilizotolewa na Shirika la Afya duniani WHO zitatumiwa.
Kulingana na matabibu katika hospitali kuu ya Mbale, waathirika ambao wametengwa na kuendelea kupata matibabu walitangamana mwishoni mwa wiki hii na mgonjwa ambaye baadaye alifariki.
Watu hao ni pamoja na mke wa marehemu, kaka yake, mganga wa kienyeji aliyejaribu kumtibu pamoja na muuguzi katika hospitali kuu ya mji huo.
Watu wengine zaidi ya 100 waliotangamana na mgonjwa aliyefariki wanafuatiliwa kwani mara nyingi alitumia usafiri wa umma katika juhudi za kutafuta kupata matibabu kuanzia mji huo wa Mbale hadi Kampala ambapo alilazwa kwa muda katika kiliniki binafsi kabla ya kupelekwa hospitali kuu ya Mulago alikofariki.
Soma pia:Ebola yathibitishwa Uganda, muuguzi afariki Kampala
Angalau watu 44 kati yao wametambuliwa wakiwemo wafanyakazi 30 wa afya. Akifafanua kuhusu hatua ambazo wamechukua kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo wa Ebola katibu wa kudumu katika wizara ya Afya Diana Atwine ametahadharisha umma kuzingatia taratibu zote za kuepusha maambukizi.
"Hatuhitaji kuwa hofu kwani wadau wote wamekubali kuchangia katika kudhibiti hali hii na kuhakikisha mifumo yetu ya kupigana nae bola ni bora hatutababaika na kutaweza na maisha ya waganda ni salama." Alisema
Wazazi na wanafunzi wapata hofu
Kutanganzwa kwa kuzuka kwa Ebola kumewatia wazazi na walimu, hofu na mashaka ya kuhakikisha watoto wao hawaathiriki. Baadhi wamesema.
Katika mojawapo ya hatua za kukabiliana na ugonjwa huo, wizara ya afya imetangaza kuwa itajaribisha chanjo kwa watu elf mbili hasa wale wanaodhaniwa kuwa katika hatari ya kuambukizwa.
Chanjo hiyo imetolewa na kuidhinishwa na Shirika la Afya duniani WHO ambalo hata mwaka 2022 lilitoa chanjo ya majaribio iliyosaidia sana katika kuudhibiti ugonjwa wa Ebola katika wilaya za kanda ya kati mwa Uganda.
Soma pia:Mtu mmoja afariki dunia kwa ugonjwa wa Ebola Uganda
Mwaka huo watu 55 walifariki kutokana na mripuko uliokumba wilaya nne. Katibu wa wizara ya afya ameelezea kuhusu ushirikiano wa Uganda, mashirika na wataalamu wa kimaitaifa katika mpango huo.
"hili ni suala la kimataifa na ndiyo maana tukitangaza mripuko na kuchukua hatua za kudhibiti ni kuhakikisha kuwa tishio hili haliathiri nchi zingine."
Chanjo nyingine ya majaribio ilipatiwa zaidi ya watu 3,000 katika nchi Jirani ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo kati ya mwaka 2018 hadi 2020 na inasifiwa kwa kusaidia katika kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
Ebola huambukiza pale unapogusa vitu vya majimaji vitokavyo kwa mwaathirika kama vile damu, jasho au mate. Ishara za ugonjwa huo ni homa kali, kutapika, kuendesha, maumivu ya misuli.