Watu wasiopungua 20 wafariki ajali ya ndege Sudan Kusini
30 Januari 2025Msemaji wa Mamlaka ya anga ya Sudan Kusini, amesema watu 21, wakiwemo raia wa Sudan Kusini na wageni, walikuwa kwenye ndege hiyo iliyokuwa ikitokea jimbo la Unity kwenda mji mkuu wa Juba.
Abiria walikuwa wafanyakazi wa makampuni ya mafuta waliokuwa wanarudi nyumbani baada ya kufanya kazi kwenye visima vya mafuta. Sababu ya ajali bado haijafahamika, lakini serikali ya jimbo la Unity ilisema inafanya kazi na makampuni ya mafuta na kampuni ya ndege kubaini majina ya wahanga.
Ajali za ndege hutokea mara kwa mara nchini Sudan Kusini, kwa sababu mashirika ya ndege hutumia ndege za zamani na zisizo na matengenezo bora. Nchi hiyo, ambayo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ina mtandao mbovu wa barabara, hivyo wasafiri hutegemea ndege kwa safari ndefu.