Watu kadhaa wauwawa katika maporomoko ya ardhi Kongo
21 Julai 2025Kulingana na walioshuhudia, maporomoko ya ardhi yalizika angalau migodi kumi na tano ya uchimbaji madini haswa dhahabu usiku wa kuamkia jumapili.
Hii jumatatu, juhudi zimeendelea ili kujaribu kupata manusura. Consolé Bafulwa ni mchimba madini anaye patikana katika kijiji cha Lomera kule Luhihi, anasema hali ni mbaya na ya kutisha.
Vyanzo vingine vinasema kwamba huenda kuna mchimbaji aliyeripua utambi, na mlipuko huo ulisababisha maporomoko ya ardhi. Msimamizi wa wilaya ya Kabare chini ya AFC/M23 Elie Rubabura ametembelea mgodi wa Lomera ili kujionea hali ya mambo.
Eneo la Lomera, sawa na shughuli nyingine nyingi za uchimbaji madini nchini Kongo, huvutia wachimbaji wengi wanaolenga kujikimu, ila mara nyingi shughuli hii inafanyika katika hali inayo hatarisha maisha yao.
Tangu kutekwa kwa jiji la Bukavu na vijiji kadhaa vya jimbo la Kivu Kusini na AFC/M23, vijana wengi, na hata baba wa familia, wamechukua hatuwa kujielekeza eneo hili la madini ili kujaribu kujikwamua kiuchumi baada ya uporaji uliotokea Bukavu muda mfupi kabla ya kuwasili kwa AFC/M23.
Kwa bahati mbaya, wengi walipoteza maisha huko kufuatia hali tete ya usalama, majanga ya asili hasa mmomonyoko wa ardhi unaotokana na uchimbaji madini usiofuata kanuni za kisasa, na hata pia kutokana na magonjwa kama vile kipindupindu.
Makundi ya waasi yasimamisha uchimbaji
Mnamo Aprili, AFC.M23 imesimamisha kwa muda shughuli za vyama vya ushirika vya uchimbaji madini katika mgodi huo.
Akiwa miongoni mwa waliosimamishwa, pia mwanasheria, Kiongozi wa chama cha ushirika wa wachimba madini wa Luhihi kwa kifupi COMILU, Nzana Namuanda Hermes anashauri mamlaka kuchukua jukumu linavyostahili ili kupunguza uharibifu mwingine katika siku zijazo :
Haya yakijiri, watu wengine wanane wamepoteza maisha kufuatia ajali ya boti iliyozama kwenye ziwa Kivu Jumamosi jioni.
Mashuhuda wanasema boti hiyo ilitoka kwenye bandari ya Kituku mjini Goma ikiwa na abiria ishirini na watatu na bidhaa kadhaa ikielekea vijiji vya Kasunyu, Luhihi na Lomera kwenye mwambao wa ziwa Kivu. Walionusurika wanasema ajali hiyo ilisababishwa na dhoruba kali.